Habari za Kitaifa

Sonko arejea kwenye siasa, atoa onyo la mapema kwa washindani

December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, ametangaza kurejea katika ulingo wa siasa baada ya kusajili chama kipya cha kisiasa cha National Economic Development Party (NEDP).

Jumanne, Bw Sonko alipokea cheti cha usajili kamili wa chama hicho, na kutangaza kuwa anawania kutawala siasa za jiji na nchi nzima kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

“Hiki ndicho chama cha kuangaliwa. Tunajenga vuguvugu litakalosaidia kuunda serikali ijayo. Msingi wetu ni mageuzi ya kiuchumi, maendeleo na kuinua maisha ya Wakenya,” alisema Bw Sonko.

Alisema chama hicho kitawakaribisha watu kutoka maeneo yote ya nchi, wakiwemo vijana wanaotarajia kuchangia kuleta mabadiliko nchini.

“Tunawakaribisha wote—kutoka Gen Z hadi wazee, kutoka misingi yote ya kisiasa—yeyote anayeamini mabadiliko ya nchi yetu. Tushirikiane kufanya kazi. Tumejikita katika kuwatumikia Wakenya,” alisema.

Ili kuvutia vijana, Sonko alitangaza kuwa kuanzia mwaka ujao, chama hicho kitazuru vyuo vikuu kuhakikisha maoni ya vijana yanazingatiwa.

Kwa mujibu wake, chama kinazingatia kusimamisha wagombeaji katika viti vyote nchini, ikiwemo urais.

“Si lazima mgombeaji urais awe Sonko. Yeyote mwenye nia ya kuwania urais anaweza kujiunga na chama, na tutatumia mchakato wa demokrasia kuamua. Tunawaheshimu Wakenya wote na hiki ni chama huru,” alisema.

Baada ya kung’olewa mamlakani mwaka 2020 na kupoteza kesi mahakamani, Sonko alisema hajakata tamaa kuhusu mchakato wake wa kupinga uamuzi huo.

“Kiongozi anaweza kuzuiwa tu baada ya kutumia kikamilifu njia zote za kukata rufaa. Mahakama ya Juu iliharakisha kesi yangu na Mahakama ya Afrika Mashariki ilithibitisha kuwa kung’atuliwa kwangu hakukuwa kwa haki, inakuwaje suala lichukue zaidi ya miaka mitatu bila mawasiliano kutolewa? Wakenya wanastahili haki, hata kutoka mahakama ya juu kabisa,” alisema.

Alisema uamuzi wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) ulipata kuwa mchakato wa kung’atuliwa kwake ulikiuka misingi muhimu ya haki, usawa na taratibu za kimahakama.

“Aidha, kwa uamuzi huo wa EACJ, sasa nitaendeleza mapambano hadi mwisho. Haki zangu zilikiukwa na ninataka  uamuzi huo uchunguzwe upya kwa sababu ukweli unaanza kujitokeza,” alisema.

Kuhusu uongozi wa chama, Bw Sonko ndiye kiongozi wa chama, akisaidiwa na manaibu wawili—Naomi Chebet Masai na Anthony Manyara. John Muchai Nyamu ndiye mwenyekiti wa kitaifa, akisaidiwa na maafisa wawili: Zablon Rashid Minyonga na Nancy Muchani.