Habari za Kitaifa

Ruto aaminia washirika wake kumletea kura 2M kutoka Mlimani

Na MWANGI MUIRURI December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

WASHIRIKA wa Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya wamebuni mpango kabambe unaolenga kuhakikisha atapata angalau kura milioni mbili kumwezesha kurejea Ikulu katika uchaguzi wa 2027.

Mpango huo unahusisha kugawa Mlima Kenya katika makundi kadhaa ya wapiga kura ili kuzuia ushawishi wa Muungano wa Upinzani katika eneo hilo.

Mnamo 2022, Rais Ruto alipata asilimia 87 ya kura za eneo la Mlima Kenya takriban nusu ya kura zote zilizompa ushindi.

Hata hivyo, tangu wakati huo uhusiano kati yake na eneo hilo umekuwa ukivurugika, hali ambayo imesababisha uhasama ikiwemo kuzomwa mara kadhaa, na migawanyiko ndani ya chama tawala cha UDA kilichowahi kushinda zaidi ya asilimia 95 ya viti katika eneo hilo.

Chanzo kikuu cha mvutano ni kung’atuliwa mamlakani kwa aliyekuwa Naibu Rais, Bw Rigathi Gachagua, mnamo Oktoba mwaka jana baada ya kuhudumu kwa miaka miwili.

Bw Gachagua sasa ameanzisha chama chake cha Democracy for Citizens Party (DCP), akikitaja kama chombo maalum cha Mlima Kenya kuzuia kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto mnamo 2027.

Bw Gachagua anaonekana kuwa tishio kubwa kwa azma ya Rais Ruto kurejea mamlakani, si tu katika Mlima Kenya bali pia kitaifa.

Ameungana na viongozi wa upinzani akiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Naibu Kiongozi wa Jubilee Fred Matiang’i na Seneta wa Kajiado Kerrar Seki kuanzisha vuguvugu la ‘Wantam’.

Vuguvugu hilo linapanga kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi kumpinga Rais Ruto 2027, huku Bw Gachagua akichukuliwa kama mhimili mkuu wa kuunganisha upinzani.

Amedai mara kadhaa kwamba “Rais Ruto anapanga kugawa Mlima Kenya kwa kuunga mkono vyama vingi vinavyomtii, kufadhili wasemaji wa jamii katika kaunti, na kutumia misaada ya pesa na chakula kama mitego ya kisiasa.”

Kwa misingi hiyo, wafuasi wa Rais Ruto wanasema wameapa “kumdhibiti” Bw Gachagua katika Mlima Kenya, wakidai ndiko anakotoa nguvu zake.

“Tunamlenga hasa huyu mtu tunayemuona kama mkabila mkuu anayejiona kama mmiliki wa Mlima Kenya,” alisema Katibu Mkuu wa UDA, Bw Hassan Omar.

Kwa upande wake, Waziri wa Utumishi wa Umma, Bw Geoffrey Ruku, amesema “Ni heri Mlima Kenya ugawanyike kuliko umoja huo kuleta hatari ya kututupa nje ya serikali.”

Alisema ushindi wa UDA katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini mnamo Novemba 27, 2025 uliwapa ari mpya.

Katika eneo lenye zaidi ya kura milioni nne, Bw Ruku anaamini kuwa takribani asilimia 47 ya kura zinaweza kutoka katika maeneo mengine na kumpatia Rais Ruto takriban kura milioni mbili.

“Tunaanza na Mlima Kenya Mashariki, Meru, Tharaka Nithi, Embu na baadhi ya Kirinyaga. Hapa ndipo ngome yetu ya kuanzisha mapambano,” alisema.

Kiongozi wa wengi katika Seneti, Bw Aaron Cheruiyott, alisema Jumapili kwamba wanachukulia Mlima Kenya kuwa mwandani muhimu wa kampeni za Ruto 2027.

Alisema madai ya Bw Gachagua kwamba “anakohoa Mlima Kenya” hayawatishi, akisema eneo hilo lina historia ya kupiga kura kwa uhuru, na lilimpatia Raila Odinga zaidi ya kura milioni moja mnamo 2022.

Mbunge wa Laikipia Mashariki, Bw Mwangi Kiunjuri, anayeratibu mikakati ya Rais Ruto eneo la Mlima Kenya, alisema mpango huo “umevuka zaidi ya asilimia 10 ya utekelezaji.”

Alisema vyama vinavyomuunga mkono Rais Ruto vitaanza kuandaa mikutano ya Baraza Kuu la Kitaifa ili kutangaza kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu ujao.

Kwa mujibu wake, endapo viongozi 300 wa ngazi ya juu watashawishi takribani wafuasi 4,000 kila mmoja, “tutaongeza kura zaidi ya milioni 1.2” kwa Rais Ruto.

Naibu Rais Kithure Kindiki, wakati wa kampeni za Mbeere Kaskazini, aliahidi kampeni kali haswa miongoni mwa vijana, akisema serikali ya Ruto “inawapatia vijana mikopo ya Sh50,000, mafunzo ya kiufundi na mitaji ya kuanzisha bishara”.

Seneta wa Embu Alexander Mundigi, alisema Prof Kindiki “anapaswa kubaki mgombea mwenza wa Ruto 2027” ili kuhakikisha Mlima Kenya unadumisha ushawishi wake ndani ya serikali.

Waziri wa Ardhi, Bi Alice Wahome, alisema wikendi kuwa “Rais Ruto atashinda 2027 kwa sababu ana timu thabiti inayofahamu uhalisia wa hali mashinani.”

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu Wachira Kiago, alitahadharisha kuwa “yanayopangwa ni michezo ya kugombania mamlaka kwa kutumia wananchi.”

Anasema Mlima Kenya unapaswa kuwa macho dhidi ya njama za kugawanywa kwa manufaa ya muda mfupi.

“Tunashikamana kwa misingi mizito kuliko siasa—damu, machozi na jasho la wapigania uhuru. Tunataka uthabiti, umoja na ustawi wa taifa,” alisema.

Aliongeza kuwa bila ushahidi wa kupambana na umaskini, ujinga na magonjwa, wapigakura wa Mlima Kenya hawatasita kujiunga na Wakenya wengine “kutafuta utawala mbadala kama wajibu wa kizalendo.”