Umuhimu wa kuchukua bima ya mimea, mifugo
MWAKA wa 2022, Kenya ilikumbwa na ukame uliotajwa kuwa mbaya zaidi kwa kipindi cha miaka 40, uliochangia hasara ya mazao na mifugo ya thamani ya mabilioni ya pesa, hasa katika maeneo kame na nusu-kame (ASAL).
Aidha, inakadiriwa kati ya mifugo milioni 2.5 na 2.6 walifariki kutokana na ukame huo.
Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Majanga (NDMA), Wizara ya Utalii, Huduma ya Wanyamapori (KWS) na mashirika kama vile IFAW na Baraza la Wakimbizi la Danish, walikadiria hasara kifedha iliyoshuhudiwa kama Sh11 bilioni.
Hasara hiyo kubwa kwa taifa, inaashiria jinsi athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyopaswa kuhamasisha wakulima kuwa na njia mbadala kulinda mimea na mifugo wao wakati wa majanga.
Bima ya kilimo na ufugaji inajitokeza kama suluhu kwenye mdahalo huu.

Mkulima Francis Kiragu anayemiliki mradi wa mifugo Kaunti ya Machakos, anakiri kuelewa maana ya bima.
Aliwahi kuhudumu katika sekta ya bima, na anataja wizi wa mifugo, kufariki kutokana na maradhi na kiangazi na ukame, kama hatari ambazo zinakodolea macho wafugaji wengi na hivyo wanapaswa kulinda wanyama wao kupitia bima.
“Nilipoanza mradi wangu wenye eneo la kunenepesha mifugo wa nyama (feedlot), jambo la kwanza lilikuwa kuhakikisha nina bima,” anasema. Aliingilia ufugaji mwaka uliopita, 2024.
Hununua ng’ombe kutoka Kaunti za Kajiado, Narok, Marsabit, Turkana na Isiolo, kisha anawaimarisha kwa siku 90 chini ya usimamizi wa daktari mtaalamu wa mifugo kabla ya kuwauza kwa wachakataji wa nyama wanaolenga masoko ya nje ya nchi.
Kulingana na Kiragu, alianza na ng’ombe 50 pekee na sasa ana mamia wanaotunzwa kwenye mradi wake.
Kwenye mahojiano na Akilimali katika warsha ya Africa Re kuhusu bima ya kilimo na ufugaji iliyofanyika Nairobi mnamo Novemba 4 na 5, Kiragu alisema hulipa wastani wa Sh4, 000 kwa kila ng’ombe kwa mwaka.
“Kiwango hicho cha bima kinafidia vifo vinavyotokana na mafuriko, ukame, magonjwa, moto na wizi,” akafichua.
Kulingana na Naibu Meneja wa Masoko ya Kilimo na Bima Africa Re Joseph Chegeh, bima huwapa wakulima ujasiri wa kuwekeza kwenye biashara ya kilimo na ufugaji, licha ya athari za tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika.
“Kenya ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na athari za tabianchi, na bila bima, sekta ya kilimo na ufugaji inakuwa uwekezaji hatari,” anasema afisa huyo.

Licha ya tija zake haswa wakati wa majanga, matumizi ya bima ya kilimo nchini bado ni chini ya asilimia moja.
Isaac Magina ambaye ni Mkuu wa Bima ya Kilimo na Tabianchi Africa Re, anasema faida zake hazipaswi kupuuzwa kwani inalinda mtandao mzima wa uzalishaji chakula.
“Karibu wakulima wadogo milioni 2 pekee ndio wana bima. Hii ni idadi ndogo sana ikizingatiwa kuwa kilimo na ufugaji ndio nguzo ya uchumi nchini,” Magina anaelezea akihimiza wakulima kukumbatia bima.
Magina anaonya kuwa madhara ya kutokuwa na bima ni makubwa.
“Wakulima wakipoteza mazao na mifugo, huzama kwenye umaskini.”
Anaongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali, sekta ya kibinafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali, ni muhimu kupunguza gharama za bima.
Wakulima wengi wanachelea kuchukua bima kwa sababu ya gharama yake ya juu.