MAONI: Viongozi wa Afrika wajiheshimu wakitaka kuheshimiwa kimataifa
IPO picha fulani ambayo siku kadha zilizopita ilisambaa mno mtandaoni ikazua mseto wa hasira, kicheko na mshtuko.
Katika picha yenyewe, Rais William Ruto na baadhi ya viongozi wa mataifa ya eneo la Maziwa Makuu walionekana wakibanana kwenye viti vya kawaida tu wakati wa ziara yao nchini Amerika.
Waliopandwa na hamaki, hasa Waafrika, walilalamika kuwa Waamerika wanawadharau viongozi wao, waliocheka wakasema ‘tamu yao’, walioshtuka wakauliza ilikuwaje viongozi hao wakakubali kubebwa kama watoto ugenini ilhali nchini kwao ni kama wafalme.
Ilinikumbusha picha nyingine ambapo viongozi wa mataifa ya Afrika walionyeshwa wakibanana kwenye viti walipobebwa kwa basi la pamoja walipohudhuria mazishi ya aliyekuwa Malkia wa Uingereza, Elizabeth.
Hiyo ya Uingereza ilizua mihemko ya kila aina, malalamiko mengi yakiwa hayo-hayo ya viongozi wa watu kutoheshimiwa ugenini, sikwambii na baadhi ya walalamishi walitishia kuwa tusipoheshimiwa tena, tutaanza kususia shughuli za uzunguni kama hizo.
Ajabu akidi ni kwamba, waliotishia kutohudhuria shughuli hizo tena ni makabwela wa kawaida tu, wengi wao hata hawajawahi kuwakilisha vijiji vyao katika shughuli yoyote, acha kusafiri nje kuiwakilisha nchi.
Lakini hiyo ndiyo hali ya mambo siku hizi, uhalisia wa maendeleo ya kiteknolojia, yaani mtandao kutukutanisha katika soko kubwa la kimataifa ambako mchunga mbuzi na kondoo nyikani anajibizana na profesa kuhusu masuala ya kimataifa, na prof wa watu hawezi kufanya kitu!
Ukijipata katika hali hiyo, jambo la hekima ni kuchagua kwa ustadi mijadala utakayoshiriki, wakati utakaposhiriki, na ni kwa kina kipi ambapo unaweza kuzama kwenye mijadala yenyewe. Na ukitukanwa na wapumbavu usikasirike, wamejaa kila mahali duniani kama hewa.
Kuhusu visa vya viongozi wetu kubebwa kama watoto, mfano kubanana kwenye viti vya kawaida tu ambavyo havina mito mizito ya kubonyea, wanaolalamika wanafichua zaidi matatizo yetu kuliko viongozi wanaotetea.
Ina maana kwamba tumekubali viongozi wetu si watu wa kawaida, wanapaswa kuchukuliwa kama viumbe maalum walio na haki ya kutunzwa kama tunu kutoka mbinguni iliyotushukia ili tuihudumie kwa namna ya kipekee.
Ina maana kwamba ubadhirifu wa viongozi wetu unakubalika kwa namna fulani hata ikiwa utatugharimu maisha bora, shule bora, afya bora, na mambo mengine ya kimsingi ambayo yalikuwa maazimio makuu ya serikali za kwanza za baada ya uhuru.
Suala la ubora wa kiti, njia ya kusafiria na mambo mengine madogo kama hayo yanamzuga akili kiumbe ambaye ama ana utoto sana, au hajafunguka mawazo kiasi cha kuelewa kuwa viti vya watu ukikalia unaviacha kwa watu, unarejea kwako kujipweteka kochini ulivyozoea.
Hayo ni mawazo ya mtumwa au mwathiriwa wa ukoloni ambaye bado hajapona kutokana na manyanyaso aliyokutana nayo minyororoni, anadhani bwana mkubwa, ajapokuwa katili wa kutupwa, yu sahihi siku zote.
Hilo ndilo tatizo kuu la mataifa yanayoendelea, yaani kuendelea kuutamani ubwana na maisha ya kipekee kwa wachache, hata ikibidi tuhatarishe maisha ya baadaye ya nchi nzima.
Hebu tafakari kuhusu kisa hicho cha hivi majuzi ambapo viongozi wetu walizuru Amerika kutia saini mkataba wa amani kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Huku viongozi wetu wakisherehekea kutia wino kwenye karastasi tu, mwenyeji wao, Rais Donald Trump, alijisifu bila kificho jinsi alivyofaulu kuitafutia nchi yake biashara ya madini maalumu yanayopatikana katika eneo hili!
Hivi una akili timamu ikiwa ulitarajia watu waliokwenda kuuza maslahi muhimu kama madini waheshimiwe na mtu aliyewarusha kibiashara? Mgongaji akuheshimu vipi tena baada ya kukucheza shere kwa urahisi namna hiyo? Heshima huja yenyewe kwa mja kujiheshimisha.
Hata hivyo, ni vyema nikwambie kuwa mataifa yaliyoendelea yalitoka huko kwa kuangalia ubora wa viti vya wageni zamani sana, sasa yako shughulini kushiriki ushindani katika viwango vya juu ambavyo Afrika tunaota kuvifikia tu.
Ngoja nikiri kitu: Hata mimi nimejipata mara kadha nikikaribia kukasirika na kulalamika kuhusu baadhi ya vitu ambavyo, kwa maoni yangu kama Mwafrika, haviendi sawa, lakini nikakumbuka huko kulitokwa.
Hivi majuzi nikielekea Israel nimesafiri kwa mojawapo ya ndege za mataifa ya Uropa, mle ndani tukapewa vijiko, uma na visu vya plastiki ambavyo vilijikatikia ovyo kila nilipotumia nguvu kiasi tu wakati wa kula. Niliudhika kidogo nikajiuliza: Yaani umaskini umemfikisha Mfaransa hapa?
Ghafla nilikumbuka nikishavitumia vitachakatwa upya kuundia vingine vya plastiki kwa gharama ndogo, hivyo hiyo ya kuyeyusha vitu na kuviumba upya nayo ni tasnia ya aina yake pia iliyowaajiri wengi.
Hali huwa hivyo hata kwenye migahawa mikubwa-mikubwa ya ughaibuni; vijiko, uma na visu vya vyuma vya kulia vinaendelea kuwa nadra, mpaka wakati mwingine unajiuliza ikiwa wameshindwa kumudu bei za vyombo vya chuma, ila unakumbuka wewe ni mpita-njia.
Kwa ufupi, acha kulalamika kuhusu wapiti-njia ambao ni viongozi wetu wanaozuru nchi za watu na kukosa starehe ambazo wamezoea kupata kwa gharama ya ushuru wangu na wako. Utasaidia zaidi ukipendekeza njia za kupunguza gharama hizo nchini. Ni suala la mtizamo tu.
– Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya anayeishi Amerika ([email protected])