Habari za Kitaifa

Upinzani: Leo ni Jamhuri Dei na tishio kubwa kwa mali ya Kenya ni Ruto

Na KEVIN CHERUIYOT December 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MUUNGANO wa Upinzani umeendelea kukosoa utawala wa Rais William Ruto, ukidai Kenya haiko salama chini ya uongozi wake, huku Wakenya wakiadhimisha miaka 62 tangu nchi ilipopata uhuru.

Katika taarifa ya pamoja Alhamisi, viongozi hao walikosoa jinsi serikali inavyoshughulikia masuala ya kitaifa na kudai Rais hana heshima kwa utawala wa sheria.

Kiongozi wa Democratic Action Party–Kenya Eugene Wamalwa, aliyesoma taarifa hiyo, alisema uhuru wa Kenya haukutolewa kama zawadi bali ulipatikana kwa damu, jasho na ujasiri wa kupigiwa mfano.

“Uhuru ulipatikana kwa kujitolea. Kila simulizi, kila jina na kila maisha yaliyopotea ni funzo kwetu leo. Hatupaswi kusahau kwamba jamhuri ni mali ya wananchi na ni wajibu wetu kuilinda,” alisema Bw Wamalwa.

Upinzani ulisema miaka 62 baada ya uhuru, Kenya iko katika hatari ya kupoteza mali na rasilmali zake chini ya utawala wa Kenya Kwanza.

Kauli zao zinakuja huku mjadala ukizidi kushika kasi kuhusu pendekezo la kuuza asilimia 15 ya hisa za serikali katika Safaricom kwa kampuni ya Afrika Kusini, Vodacom.

“Rasilmali za kitaifa kama Safaricom, Kenya Pipeline, KCB na JKIA zimekuwa zikilengwa, zikidhoofishwa na kuuzwa bila uwazi, bila ushirikishaji wa umma na bila kuzingatia sheria na katiba,” alisema Bw Wamalwa.

Kwa mujibu wa Upinzani, baadhi ya mali hiyo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi na inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote.

“Haya sio mageuzi ya kiuchumi. Huu ni ukoloni mamboleo wa kimataifa, mchakato wa kimya kimya wa kuuzwa kwa mamlaka yetu ya kitaifa.”

Walitangaza kuwa tayari wamefikisha suala hilo mahakamani wakitaka kusitishwa kwa mpango wa kuuza sehemu ya hisa za serikali katika kampuni ya Safaricom.

“Lengo la serikali hii lilikuwa wazi: ni kupunguza kwa hatua moja baada ya nyingine mamlaka ya nchi.”

Aidha, waliitaka serikali kuwachukulia hatua waliohusika na vurugu wakati wa uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni.

Bw Musyoka alisema Muungano wa Upinzani uko tayari kushtaki maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wakiwamo mwenyekiti Erastus Ethekon na Afisa Mkuu Mtendaji Marjan Hussein Marjan.

“Hatutaruhusu nchi hii iuzwe,” alisema.

Kiongozi mwenza wa Upinzani, Bw Gachagua, alidai Wakenya wameungana kupinga ukandamizaji, umasikini na maovu ambayo amesema yamesababishwa na serikali ya Rais Ruto.

“Tatizo la Kenya ni wizi wa mali ya umma, ufisadi wa kupindukia, matumizi mabaya ya rasilmali, dharau kwa sheria, utekaji nyara wa watu, mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria na hongo waziwazi katika Ikulu,” alisema, akiongeza kuwa masuala ya ukabila yanatumika kupotosha umma ili wasijadili shida za kweli.

Migawanyiko inayoendelea ndani ya Muungano wa Upinzani imeibua maswali kuhusu uthabiti wa kundi hilo kuelekea uchaguzi wa 2027, hasa kutokana na kukosekana mara kwa mara kwa viongozi wakuu katika mikutano ya hadhara.

Kiongozi wa People’s Liberation Party (PLP), Martha Karua, amekuwa akikosa mikutano, sawa na Dkt Fred Matiang’i wa chama cha United Progressive Alliance (UPA).

Viongozi hao hawakuhudhuria kikao cha Alhamisi ambapo taarifa ya Upinzani ilisomwa jijini Nairobi kabla ya sherehe za Jamhuri Day.

Hata hivyo, Bw Kalonzo Musyoka, Bw Gachagua na Bw Wamalwa walisema bado wako pamoja nao licha ya kukosekana kwao.

“Kila mara tumekuwa pamoja. Mmeona hata Januari 22 tulipoanza safari hii, Dkt Matiang’i hakuwa lakini alimtuma Seneta Onyonka. Leo pia ametuma Gloria Orwoba,” alisema Bw Wamalwa.