Makala

Ngoma ya ‘Mwazindika’ kutoka Taita yatambuliwa na UN

Na ANTHONY KITIMO December 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NGOMA ya kitamaduni ya jadi ya Taita Taveta inayojulikana kama ‘Mwazindika’ imetambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na itakuwa ikilindwa kimataifa kupitia kwa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Tangazo hilo lilifanywa katika mkutano wa shirika hilo uliofanyika Desemba 9 nchini India, ambapo UN ilitangaza kushirikiana na Kaunti hiyo na taasisi zingine ili kulinda ngoma hiyo.

Ngoma hiyo, ambayo imekuwa ikipingwa na viongozi wa dini hasa makanisa, huchezwa na wanaume na wanawake, hasa wakati wa sherehe kama vile harusi, mazishi, na tamasha zinginezo.

Aidha, huonyesha utamaduni wa jamii hiyo, pamoja na historia yao, maadili, na kanuni za kijamii.

Wakati wa kucheza ngoma hiyo, wanaoshiriki husisimuka kiasi kwamba wakati mwingine huonekana kupagawa, hasa wakati ngoma inapopigwa.

Wakati wa kucheza nyimbo za Mwazindika, wanaoshiriki hutumia ngoma kubwa zilizotengenezwa kwa shina za miti zilizochimbwa, zikipambwa kwa ngozi ya ng’ombe na shanga na vilevile kupiga firimbi na vigelegele.

Wachezaji huvaa kofia za aina ya kipekee vichwani, mikufu, bangili, na vikuku vya miguu.

Bw Mwaliko wa Maghenda, mmoja wa wazee wa Taita, alisema ngoma hiyo imekuwa ikididimia kutokana na vijana kuhamia mijini pamoja na kutozingatia mila na desturi.

“Kukumbatia dini na vijana wengi kuhamia mijini ni mmoja ya sababu ambazo tunaona ngoma hiyo inazidi kudidimia, wazee wanakufa ilhali vijana hawataki kufunzwa jinsi ya kuicheza. Vilevile, wakazi wengi wamezingatia dini na kushirikisha ngoma hiyo na uchawi na utamaduni,” alisema Bw Maghenda.

Wakati wa kuorodheshwa, naibu gavana wa Taita-Taveta Christine Kilalo, alisema ni fahari kubwa kwani Unesco itasaidia kupitisha ujuzi huo kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

“Kwa kurekodi ngoma hiyo, Mwazindika itaweza kutangazwa kote nchini na kuvutia watalii wengi katika Kaunti yetu hivyo kuwanufaisha watu wetu kiuchumi,” alisema Bi Kilalo.

Mchakato wa kuorodhesha ngoma hiyo ulianza Februari 20, 2024 ambapo wataalamu wa Unesco, wakiongozwa na mshauri wa utamaduni wa ukanda wa Afrika Mashariki Masanori Nagaoka na Mkurugenzi wa Utamaduni wa Tume ya Kitaifa Julius Mwahunga, walizuru kaunti hiyo ili kushirikiana na wadau mbalimbali kuhusu mchakato wa kuandikisha ngoma hiyo.

Wajumbe hao walikutana na maafisa wa serikali na wale wa taasisi mbalimbali, wachezaji wa Mwazindika kutoka makundi tofauti, na baraza la wazee kutoka sehemu mbalimbali za kaunti.

Siku ya Jumatatu, katika kikao maalumu cha 20 cha mwaka mwenyekiti wa ujumbe maalumu wa unesco Vishal V. Sharma, alitangaza kuidhinishwa kwa hoja hiyo baada ya kujadiliwa na ujumbe katika makao makuu ya umoja wa Mataifa Paris Oktoba 23, 2025.

Kwa kuidhinishwa, ngoma hiyo italindwa na kukuzwa na Unesco kwa kuihifadhi na kurekodi ngoma hiyo, ili kupitishwa kutoka kizazi hadi kizazi kingine,” alisema Bw Sharma.