Wasichana wabwaga wavulana kwenye matokeo ya mtihani wa kwanza, KJSEA
WASICHANA waliibuka kidedea dhidi ya wavulana katika matokeo ya mtihani wa kwanza wa Gredi 9 KJSEA yaliyotangazwa Alhamisi, Desemba 11, 2025 na Waziri wa Elimu Julius Ogamba.
Waziri alisema kati ya wanafunzi 1,130,459 waliotahiniwa katika mtihani wa KJSEA 2025, wavulana walikuwa 578,630, huku wasichana wakiwa 551,829, sawa na asilimia 51.19 na 48.81 mtawalia.
Wasichana waliwashinda wavulana katika masomo 10 kati ya 12 kwa viwango vya Kutimiza Matarajio na Kuzidi Matarajio.
Tofauti kubwa zaidi ilionekana katika Kiswahili (asilimia 64.8 dhidi ya asilimia 51.), ikifuatiwa na Somo la Dini ya Kikristo (asilimia 59.77 dhidi ya asilimia 48.39), Kiingereza (asilimia 52.86 dhidi ya asilimia 48.45), na Somo la Kijamii (asilimia 62.98 dhidi ya asilimia 54.35).
Hata hivyo, masomo ya Hisabati na Lugha ya Ishara ya Kenya yalitia wasiwasi, kwani ni asilimia 32.44 na asilimia 22.14 pekee ya wanafunzi mtawalia waliotimiza au kuzidi matarajio.
Kati ya wanafunzi wote 1,130,459, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 59.09 wana uwezo wa kujiunga na mkondo wa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) katika shule za upili, asilimia 46.52 wanafaa mkondo wa Sayansi ya Jamii, huku 48.73 wakionyesha uwezo wa kuendelea na mkondo wa Sanaa na Michezo.
“Tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Tathmini inayolenga umilisi, utendaji wa wanafunzi umezingatia viwango vya Kuzidi Matarajio, Kutimiza Matarajio, Kukaribia Matarajio na Chini ya Matarajio,” alisema Waziri Ogamba.
Alisema katika mtihani wa KJSEA, mfumo umefuata mkondo huo huo, ambapo kila kiwango kimegawanywa zaidi ya mara mbili na hivyo kuunda ngazi nane.
Matokeo ya KJSEA yametolewa kwa kiwango cha alama kutoka 1 hadi 8, ambapo alama 8 ndiyo ya juu zaidi (Kuzidi Matarajio 1) na alama 1 ndiyo ya chini zaidi (Chini ya Matarajio 2).
Waziri alisema viwango hivi vinalenga kutofautisha kati ya utendaji bora kabisa na utendaji mzuri.
Kaunti zilizoandikisha idadi kubwa zaidi ya watahiniwa ni Nairobi (71,022), Kakamega (59,384) na Nakuru (54,028).
Kaunti 41 ziliripoti idadi kubwa ya watahiniwa wa kiume kuliko wa kike, huku Mombasa ikiwa kaunti ya pekee iliyofikia usawa wa kijinsia wa asilimia kwa wavulana na wasichana.
Kaunti tano—Isiolo, Nairobi, Samburu, Marsabit na West Pokot—zilikuwa na idadi kubwa zaidi ya wasichana kuliko wavulana.
Kwa jumla, wanafunzi 642,620 (asilimia 56.84) waliokuwa katika umri ufaao wa miaka 14–15 ndio waliofanya mtihani huo.
Watahiniwa waliokuwa na umri mdogo (miaka 13 na chini) walikuwa 35,270 (asilimia 3.12), ilhali wenye umri wa 16–17 walikuwa 415,059 (asilimia 36.71).
Watu wazima wenye umri wa miaka 18 na zaidi walikuwa 37,638 (asilimia 3.33).
Kaunti ya Kilifi ilisajili idadi kubwa zaidi ya watahiniwa waliozidi umri ufaao (miaka 16 na zaidi) kwa asilimia 64.90, ikifuatiwa na Kwale (asilimia 64.78), Garissa (asilimia 63.38), Taita Taveta (asilimia 62.06) na Mandera (asilimia 62.05).
Kwa upande mwingine, Baringo ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa zaidi ya watahiniwa wenye umri mdogo (miaka 13 na chini) kwa asilimia 10.10, ikifuatiwa na Bomet (asilimia 7.56), Marsabit (asilimia 7.48), Narok (asilimia 7.28), na Kericho (asilimia 7.25).
Kati ya masomo 12 ya KJSEA, masomo 7 yalirekodi kiwango cha juu cha wanafunzi waliotimiza na kuzidi matarajio.
Haya ni: Dini ya Hindu (asilimia 84.62), Sayansi Jumuishi (asilimia 61.77), Somo la Kijamii (asilimia 58.56), Sanaa ya Ubunifu na Michezo (asilimia 58.04), Kiswahili (asilimia 57.98), Dini ya Kikristo (asilimia 53.9), Kilimo (asilimia 52.26).
Asilimia 75 ya wanafunzi walipata alama za Kukaribia Matarajio (AE) na juu katika masomo yote huku Sanaa ya Ubunifu na Michezo likiibuka kuwa somo lililofanya vyema zaidi kwa asilimia 96.84, likifuatiwa na Kilimo (asilimia 96.254), Kiswahili (asilimia 93.11) na Somo la Kijamii (asilimia 92.93).
Daraja la AE linatosha kumwezesha mwanafunzi kuendelea na mkondo wa elimu ya sekondari unaohitaji uwezo wa msingi katika somo husika.