Habari za Kaunti

Wajawazito wanne walala kitanda kimoja hospitali ya Margaret Kenyatta ikilemewa

Na ERIC MATARA December 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HOSPITALI ya Mama na Watoto ya Margaret Kenyatta jijini Nakuru ambayo ni ya pili kwa ukubwa ya aina hiyo nchini baada ya Pumwani jijini Nairobi, inakabiliwa na msongamano mkubwa ambapo hadi akina mama wanne pamoja na watoto wao wanalazimika kutumia kitanda kimoja.

Hospitali hiyo yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 250, iliyoko ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Nakuru Level Five, imefurika kupita kiasi.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa vitanda vilivyo katika wadi havitoshi kuhudumia idadi kubwa ya wanawake wanaotafuta huduma za kujifungua.

Ingawa jengo hilo la kisasa linaonekana maridadi kwa nje, hali ya ndani ni ya kusikitisha na imeendelea kudorora, na kuwaacha wagonjwa katika hali ya kukata tamaa.

Akina mama wajawazito na waliojifungua hulazimika kulala kwa zamu, huku wengine wakilala sakafuni kutokana na ukosefu wa vitanda.

Kutokana na msongamano mkubwa, akina mama watatu na watoto wao wachanga hutengewa kitanda kimoja, na mara nyingine hadi wanne.

“Hali hairidhishi kabisa,” walisema akina mama waliolalamika walipoongea na Taifa Leo.

Ziara za hivi karibuni katika wadi ya uzazi zilionyesha kuwa tatizo hilo limekuwepo kwa muda mrefu, bila ishara yoyote ya hatua ya dharura kuchukuliwa.

Mama mmoja, Velyn (si jina lake halisi), anayemlea mtoto mchanga katika kituo hicho, aliambia Taifa Leo kuwa yeye na akina mama wengine watatu wamelazimika kutumia kitanda kimoja wakati wote alikuwa hapo.

“Tunalala kwa zamu. Wakati mwingine tunalala kitanda kimoja watu wanne, na wengine hulala sakafuni. Unatumia nguo na leso zako kujifariji kwa sababu hakuna mashuka wala magodoro ya kutosha,” alisema.

“Wakati mwingine tunakesha usiku kucha ili tu watoto wetu wapate kulala,” akaongeza.

Kitengo hicho ambacho kinapaswa kuwa mahali salama kwa wajawazito sasa kinawaweka katika hatari ya kuambukizwa maradhi kutokana na msongamano mkubwa.

Muuguzi mmoja katika kituo hicho, ambaye hakutaka kutajwa, alifichua kuwa kutokana na wingi wa wajawazito wanaowasili, mara nyingi hulazimika kutandaza vitanda vya dharura sakafuni au kuwaweka akina mama kwa pamoja kitandani.

“Idadi ya wajawazito imekuwa ikiongezeka sana miezi ya karibuni na wakati mwingine hatuna chaguo ila kuwaweka akina mama pamoja. Hatuwezi kuwakataa waliofika tayari kujifungua,” alisema muuguzi huyo.

Wakazi na wanaharakati wa mashirika ya kiraia sasa wanaitaka serikali ya Kaunti ya Nakuru kuchukua hatua za haraka kuboresha hali katika wadi hiyo ili kuepuka hatari ya maambukizi.

Maafisa wa afya wamethibitisha uzito wa tatizo hilo, wakisema linatokana na wagonjwa kuwa wengi.

Mnamo Jumatatu jioni, maafisa wa Afya wa Kaunti ya Nakuru walikiri kuwepo kwa msongamano, wakidai unatokana na idadi kubwa ya watu wanaotegemea hospitali hiyo.

“Idara ya afya inataka kutoa ufafanuzi kuhusu wasiwasi ulioibuliwa kuhusu msongamano katika Kitengo cha Mama na Mtoto cha Margaret Kenyatta ndani ya Hospitali ya Nakuru Level Five. Kama hospitali ya rufaa inayohudumia Nakuru na zaidi ya kaunti sita jirani, wakati mwingine shinikizo la mahitaji na matarajio ya huduma huongezeka,” alisema Waziri wa Afya wa Kaunti ya Nakuru, Bi Roselyn Mungai.