Akili Mali

Anaagiza malazi ughaibuni na kuwauzia wateja Afrika Mashariki

Na PETER CHANGTOEK December 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LILIAN Kemunto, almaarufu Kiki au Kiki The Lioness, amekuwa akifanya biashara ya kuagiza na kuuza malazi kutoka ughaibuni kwa muda wa miaka 12, na hana nia ya kuiacha biashara hiyo asilani.

Mjasiriamali huyo amekuwa akiziagiza bidhaa hizo kutoka nchini Canada, na kuwauzia wateja wake walioko Afrika Mashariki. Kampuni yake inajulikana kama Kiki’s Mall, na iko jijini Mombasa.

Kemunto anasema kwamba, alianza kwa kuutumia mtaji ambao haukuwa mwingi mno, na kuwekeza faida alizokuwa akipata kwenye biashara hiyo, nayo ikanoga na kunawiri.

Wakati anapoziagiza bidhaa hizo, Kemunto hushurutika kusafiri hadi mahali ambako bidhaa hizo hutengenezwa, ili kuhakikisha kuwa anazinunua bidhaa zenye ubora wa kiwango cha juu.

Alijitosa katika biashara hiyo baada ya kuliona pengo katika uagizaji wa biadhaa kama hizo, na akaamua kulijaza pengo hilo. Anasisitiza kuwa, brandi yake inazingatia starehe kwa wateja, umaridadi wa bidhaa hizo, na bei ambazo wateja wanamudu.

“Naamini kuwa kila mtu huhitaji usingizi mwanana. Kwa kuwa malazi hutumika kila siku nyumbani, hotelini, hospitalini, na shuleni, niliona fursa ya kipekee kutoa bidhaa bora ili kuboresha starehe kwa watu. Kenya ilikuwa na bidhaa chache za malazi yenye ubora, ya kudumu, na yaliyotengenezwa kwa ubora – kwa hivyo, nikaamua kujaza pengo,” asema mfanyabiashara huyo.

Hapo awali, alikuwa akiagiza bidhaa ambazo ni mitumba. Hata hivyo, aliamua kuziagiza bidhaa mpya zilizotengenezwa kwa ubora wa juu, ili kuwavutia wateja wengi zaidi.

“Kwa wakati huu, tunaziagiza na kuziuza bidhaa zinazotengenezwa katika viwanda, zinazoleta mvuto kwenye makazi. Bidhaa zetu zote zimetengenezwa kuambatana na mapambo ya ndani ya makazi,” aongeza.

Shughuli ya kuziagiza bidhaa hizo huchukua muda wa takribani miezi mitatu hadi mitano, hadi wakati zinapowasilishwa nchini. Wakati wa uagizaji, Kemunto husafiri hadi kwa viwanda kwa nchi inayotengeneza bidhaa hizo.

Lilian Kemunto aonyesha baadhi ya bidhaa anazoziagiza kutoka ughaibuni, na kuziuza jijini Mombasa. PICHA|PETER CHANGTOEK

“Hatuagizi kupitia kwa mitandao,” asema, akiongeza kuwa, mchakato mzima unahitaji mtu awe katika eneo ambako bidhaa hutengenezwa ili kupata bidhaa bora.

Husafiri kwa mara ya pili wakati bidhaa hizo zinapotengenezwa, ili kuhakikisha ni bora, na kuhakikisha kuwa stakabadhi za kusafirisha bidhaa ziko sawa. Kufanya hivyo kunasaidia bidhaa kufika kwa wakati, na kuepeka hatari ya kuharibika au kupotea kwa bidhaa.

Hakuna jambo lisilo na changamoto. Mfanyabiashara huyo anasema kuwa, kuna changamot kadhaa katika biashara hiyo. Mojawapo ya changamoto hizo ni kodi za juu za uagizaji wa bidhaa kutoka nje. Aidha, kupanda na kushuka kwa thamani ya Dola ya Marekani ikilinganishwa na Shilingi ya Kenya, ni changamoto nyingine.

Pia, hulipia ada za juu kusafirisha bidhaa kutoka nje. Isitoshe, wakati mwingine bidhaa huchelewa kuwasili. Hata hivyo, changamoto hizo humtia nguvu zaidi.

“Wateja wetu ni wauzaji wa rejareja, hoteli, na wamiliki wa nyumba. Tunawafikia kupitia kwa mitandao ya kijamii kama vile Facebook (Kiki’s Mall), Instagram, WhatsApp Business, TikTok. Hupakia picha na video kila siku, pamoja na ushuhuda wa wateja,” asema.

Mjasiriamali huyo anasema kuwa, huuza robota la mashiti yaliyo na umaridadi kwa Sh30,000 (jozi 20) each, robota lenye bidhaa zilizochanganywa Sh30,000 (jozi 20) kila moja, robota la mfarishi (duvet) huuzwa kwa Sh26,000 (seti 10) kila moja.

“Tunauza duvet cover robota moja kwa Sh49,000 (seti 20), kila jozi (pair) lina mashiti mawili na foronya nne (pillowcases 4),” aongeza.

Mbali na malazi, mjasiriamali huyo pia huagiza bidhaa kutoka China. Aidha, huagiza bidhaa za urembo kutoka Marekani, samani za kiwango cha juu, pamoja na viatu.

Ana wafanyakazi wanne kwenye idara ya mashiti, na wengine 20 wanaomsaidia wakati bidhaa zinapowasilishwa.

Kemunto, anayepania kupanua biashara hiyo, kwa kuanzisha madukakuu kote nchini, anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika biashara kuanza na mtaji wowote.