Huyu hapa mchezaji hodari wa Fidla na Gofu
SHAY Jinal Shah, ni mwanafunzi katika Shule ya Mombasa Academy, ambaye ana tajriba kubwa mno katika upigaji fidla.
Aidha, ni mchezaji hodari wa gofu, na amecheza nje ya Kenya.
Shay, ambaye ana umri wa miaka 10, alishikilia nafasi ya pili kitaifa, katika Tamasha za Muziki za 2024, katika upigaji wa fidla.
Anadokeza kwamba, anapania kuwa mchezaji tajika wa fidla katika siku za usoni.
Kabla hajatambulika kama mchezaji hodari wa fidla, alitumia nafasi yake kuwatazama wachezaji hodari wa fidla, kama vile Antonio Vivaldi na Ray Chen, kupitia YouTube.
“Baada ya kumtazama Ray Chen kwa YouTube, na kutazama video zake, alinipa motisha ya kucheza fidla,” asema mvulana huyo.
Mbali na kutumia YouTube kukinoa kipawa chake cha kupiga fidla, mwelekezi wake, Joyce Mueni, amekuwa akimsaidia kukikuza kipaji hicho zaidi.
Shay alitia bidii mno katika mashindano kuanzia kwenye ngazi mbalimbali – kaunti ndogo, kaunti na hadi akafikia kiwango cha kitaifa, ambapo alishiriki katika mashindano hayo na kuwa wa pili.
“Nilishiriki katika mashindano matatu kabla ya kushiriki katika mashindano ya kitaifa ya Tamasha za Muziki za Kenya 2024. Nilishiriki katika kaunti-ndogo, kaunti, na katika jimbo, na katika kiwango cha kitaifa,” asema Shay.
Kabla ya kushiriki kwenye mashindano hayo, mwanafunzi huyo alikuwa akifanya mazoezi kila wakati ili kuhakikisha kwamba anafanikiwa kuwa katika nafasi bora kwenye mashindano.

“Nilikuwa nikifanya mazoezi huku nikiwaza kuhusu mbwa wangu anayejulikana kama Fluffy, ili kutuliza akili. Hata nilishangaa kuwa miongoni mwa tano bora na nikawa na fahari na furaha kwa kufanya vyema, kwa sababu kuliwa na washiriki waliokuwa na tajriba,” aeleza Shay.
Anadokeza kuwa, alikuwa akifanya mazoezi kwa ajili ya tamasha hizo za muziki, huku akidurusu matini kwa ajili ya mtihani wake.
“Nilikuwa nikifanya mazoezi kila baada ya siku mbili, kwa muda wa karibu saa moja, kwa sababu nilikuwa nikijiaandaa kwa ajili ya mtihani. Mazoezi yalikuwa magumu, kwa sababu nilikuwa nikishughulika na matini, huku nikilazimika kuwasha fidla kila mara,” asema.
Shay anasema kwamba, anapopiga fidla, huhisi kana kwamba akili yake inatulia. Anasema kuwa, ataendelea kufanya mazoezi ya kupiga fidla hadi awe mtaalamu wa zana hiyo.
Anafichua kwamba, amekuwa akipata usaidizi wa kukikuza kipaji chake cha upigaji fidla kutoka kwa wazazi wake, mwelekezi wake, pamoja na shule kwa ujumla. “Wao hunitia moyo kila wakati, kwa kunifanya niwe na mtazamo chanya na kunishauri nijiamini,” asema Shay.
Mueni, ambaye ni mwelekezi wa Shay, anasema kuwa, kujitolea kwa Shay wakati wa mazoezi, kulimpa matumaini kuwa angefanya vyema kwenye tamasha za muziki.
“Matokeo yalipotangazwa, nilikuwa na furaha kupita kiasi. Nilikuwa nikitarajia afanye vyema,” asema.
Mbali na kuwa mpigaji hodari wa fidla, mwanafunzi huyo pia ni mchezaji shupavu wa mchezo wa gofu.
Alikuwa wa tatu katika mchezo wa gofu wa US Kids Coast Tour 2022.
Mchuano huo ulimfanya atambulike na kuenda kucheza nchini Uganda, kwa mashindano ya US Kids, 2023, akiwakilisha Kenya. Katika mchuano huo, Shay alishikilia nafasi ya tatu kwa mara nyingine.
Shay, alicheza msimu wa mwaka 2024, ambapo amechezea Vipingo, na kuwa wa pili.
Klabu yake ya nyumbani ni Nyali Golf na Country Club.
Katika msimu wa Desemba, atashiriki katika US Kids, na atakuwa akishiriki katika mchuano wa Golf Handicap mwezi huu wa Desemba.
Amefanya mtihani wa Gredi ya 2 ya ABRSM wa fidla, na anasubiri matokeo. Mbali na kupania kuwa tajika katika upigaji fidla katika siku za usoni. Shay pia anatarajia kuwa mchezaji hodari wa gofu, na kucheza PGA.