Mkutano wa Sifuna, Osotsi na Wazee waibua maswali
WAZEE wa jamii ya Waluhya wanaonekana kuingilia suala la umoja wa jamii hiyo huku maswali yakiibuka kuhusu kujitolea kwao kutokana na kile kinachotajwa kama kuegemea mrengo mmoja.
Mnamo Alhamisi, Desemba 11, 2025, Wazee hao walifanya kikao cha mashauriano na viongozi wakuu wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kutoka eneo la Magharibi ili kujadili mustakabali wa jamii hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
“Si mara ya kwanza kwa watu mashuhuri kusaka umoja wa jamii ya Mulembe na kila wakati huwa wanagonga mwamba kwa kutokuwa na mikakati inayoleta pamoja viongozi wote. Mara nyingi azma hiyo huwa ya maslahi ya mrengo mmoja wa kisiasa au ya kibinafsi,” asema mchanganuzi wa siasa Musili Koli.
Wazee hao walikutana na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna na Naibu Kiongozi wa chama hicho, Godfrey Osotsi, wakitaka kufahamu nafasi ya jamii ya Waluhya ndani ya ODM baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, marehemu Raila Odinga.
“Tuliwaita viongozi hawa wawili wakuu wa ODM watupe taarifa kuhusu yanayoendelea ndani ya chama. Sehemu kubwa ya jamii yetu iko ODM. Kwa hivyo, kinachoendelea humo kinatuhusu,” alisema Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wazee wa Luhya, Fred Omindo na kuongeza kuwa mkutano huo ni sehemu ya juhudi za jamii kuungana upya kabla ya uchaguzi wa 2027 kutokana na kugawanyika kwao kisiasa mara kwa mara, hali inayowanyima nguvu katika majadiliano kitaifa.
Hata hivyo maswali yameibuka kuhusu wanavyoshughulikia suala hilo, nia yao na kwa nini hawahusishi viongozi wote kutoka ukanda huo bila kujali mirengo yao ya kisiasa.
Japo wanasema wanataka ushirikishaji wa jamii na uwajibikaji katika shughuli zinazogusa eneo hilo ukiwemo uchimbaji dhahabu na kukodishwa kwa viwanda vya sukari, wachambuzi wanahisi wangepanua wigo na kuhusisha viongozi kutoka mirengo tofauti ya kisiasa.
Miongoni mwa wazee hao ni Patrick Wangamati, Noah Wekesa, Fred Omido, na Peter Ludava.
Maswali yameibuka kuhusu kwa nini hawakuitisha kikao cha pamoja cha viongozi kutoka vyama vingine ambao wamekuwa wakilalamikia jinsi serikali inavyoshughulikia masuala na rasilmali za eneo la Magharibi.
Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, ameshikilia msimamo wake kuhusu mvutano wa dhahabu Ikolomani, akisisitiza kuwa rasilmali za eneo hilo ni mali ya wananchi na hakuna kampuni, iwe ya ndani au ya kigeni inayopaswa kuchimba bila uwajibikaji na uwazi.
Khalwale aliongeza kuwa ajira kwa vijana, utunzaji wa mazingira, na uwajibikaji wa wawekezaji lazima viwe kipaumbele katika shughuli za uchimbaji.Sifuna aliweka wazi kuwa “rasilmali za Kakamega ni mali ya wananchi, na hatutaki mtu yeyote afaidike kwa siri huku vijana wetu wakiwa hawana ajira na vijiji vyetu vikisalia bila maendeleo.”
Wachambuzi wa siasa wasema kuwa kutengwa kwa baadhi ya viongozi hasa wa upinzani katika kikao hiki kunazua maswali.
‘Kuandaa kikao cha viongozi wakuu wa chama kimoja kunaonyesha wazee wana lengo ambalo linaegemea upande mmoja. ODM iko ndani ya Serikali Jumuishi na ndicho chama kikubwa Magharibi mwa Kenya. Kualika viongozi wake wakuu kutoka eneo hilo pekee kunazua maswali kuhusu hasa mpango wa wazee hao,” anasema mchambuzi wa siasa Dkt Jeff Omondi.
Anashangaa walikokuwa wazee hao wakati kampuni za sukari zilikuwa zikibinafsishwa ndipo wajitokeze sasa hivi wakati joto la kisiasa linaanza kupanda kufuatia mzozo wa dhahabu na uchaguzi mkuu unapokaribia.
Anasema mkutano huu unaashiria kuna mpango kati ya wazee hao na baadhi ya wanasiasa. Anaongeza kuwa iwapo ni kwa maslahi ya eneo na kulinda rasilmali, mkutano unafaa kuhusisha viongozi wote kwa nia njema na si kutumiwa kuendeleza maslahi ya wachache kwa kujifanya kutetea jamii.
“Muhimu ni umoja wa jamii ya Magharibi ambao umekuwa ukiyeyuka hata kabla ya kuiva,” asema.
Wazee hao walisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na ushirikishaji wa umma katika shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika maeneo ya Ikolomani na Vihiga ambapo kampuni ya Shanta Gold inakusudia kufanya shughuli hiyo.
Pia, waligusia sekta ya sukari, wakikosoa jinsi viwanda vya Mumias na Nzoia vinavyoendeshwa jambo ambalo linaweza kuwa na madhara kwa ustawi wa vizazi vijavyo vya jamii ya Waluhya.
Wazee waliongeza kuwa wanakusudia kushirikiana na Baraza la Jamii ya Waluo katika kutatua tatizo la ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi.