Habari

Waziri atetea matokeo ya KJSEA akisema mfumo wakuza talanta

Na NDUBI MOTURI December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Elimu Julius Migos amepongeza matokeo ya mtihani wa KJSEA yaliyotolewa Alhamisi, akisisitiza kuwa mfumo mpya umeundwa kuwapa wanafunzi nafasi ya kukuza talanta zao badala ya kuwafunga kwenye matokeo ya masomo pekee.

Akizungumza katika sherehe ya shukrani ya Sabato jijini Nairobi kwa jamii ya Abagusii iliyofanyika jana, Bw Migos alitetea mfumo wa tathmini unaozingatia umilisi, akisema umeleta uwazi, ushirikishaji na karibu wanafunzi wote waliofanya KJSEA watajiunga na sekondari pevu.

“Tuliwaambia Wakenya kwamba, kati ya wanafunzi 1,130,000 waliofanya mtihani, tulikuwa na visa saba tu vya udanganyifu katika masomo mawili kutoka shule mbili,” alisema.

Kwa mujibu wa waziri, wote waliofanya mtihani watajiunga na sekondari pevu.

‘Wanafunzi wote, wahitimu wote, watakuwa darasani ifikapo Januari 12, 2026,’ aliongeza, na kusema wasiwasi kutoka kwa wazazi na walimu kuhusu kasi ya mabadiliko ilikuwa inatarajiwa.

‘Wale wote wanaoshindwa kubadilika na mfumo mpya, itachukua muda, lakini tutafika huko.’

Bw Migos alikataa dhana ya kushindwa katika mfumo mpya wa alama, akieleza kuwa mtihani huo umeundwa kupima maendeleo ya mwanafunzi binafsi badala ya kuwaweka wanafunzi kwenye mashindano na wenzao.

‘Wote waliofanya mtihani huu walifaulu,’ alisema.

‘Kiwango sasa ni kuzidi matarajio, kutimiza matarajio na cha tatu ni kukaribia matarajio. Kiwango cha mwisho ni chini ya matarajio. Muhimu ni kwamba, tunajaribu kupima matarajio ya kila mmoja. Hivyo huwezi kusema kuna mtu ameshindwa.’

Alisema mfumo huo unawawezesha wanafunzi kufuata mikondo mbalimbali kulingana na nguvu zao, ikiwa ni pamoja na sanaa na sayansi ya kijamii, sayansi na teknolojia, au michezo.