KINAYA: Wanaume wazuiwe kuchagua ‘mama kaunti’ almaarufu ‘Woman Rep’
EWE ndugu yangu ‘Chautundu’, weka kando matusi, dharau na utundu unijibu swali hili: Hivi umewahi kumwangalia mwanasiasa fulani akiropokwa na maneno ukajiambia kimoyomoyo ‘huyu anafaa kuwa mwakilishi wa wanawake bungeni?’
Wala sirejelei matusi yako ya kawaida ya kusema mwanasiasa fulani au fulani usiyempenda ana ‘umama’, la hasha!
Narejelea mtu yeyote ambaye anapenda vyeo sana hivi kwamba akipewa cha kuwawakilisha wanawake, yaani awe ‘mama kaunti’, yuko radhi kuvaa rinda.
Katika siasa zetu hizi zilizojaa ushindani, labda kuna mwanamume fulani ambaye anakesha usiku kucha ilhali yu macho akiwaza na kuwazua bila mafanikio, akijiuliza inawezekanaje kutwaa mojawapo ya vyeo hivyo maalum vya wanawake.
Najua kuna wanaume wengi ambao wanatamani kuwania vyeo vya wawakilishi wa kike bungeni, lakini hawana namna! Wakivaa marinda na sketi ili kupata vyeo watavua lini, tena watarejeaje kwa wananchi, hasa watakapostaafu siasa?
Kama nzi anayekuta kinyesi kikavu cha mwaka jana na kujiuliza ‘hiki kilikauka nikiwa wapi?’, baadhi ya wanaume wanajiuliza wadhifa wa ‘mama kaunti’ uliingiaje kwenye sheria zetu bila kupingwa na wanaume.
Nimewasikia wengi wakinong’onezana kuwa Kenya haifai kuwa na viti maalum ambavyo ni watu wa jinsia moja tu wanaoruhusiwa kuviwania.
Wanadai huo ni uonevu na ubaguzi wa kijinsia eti, hali Katiba ya nchi inakataza ubaguzi wa aina yoyote ile.
Wapo wanaohakiki michango ya ‘mama kaunti’ wote waliowahi kuchaguliwa tangu mwaka 2013 na kujiambia wanaweza kufanya kazi bora zaidi kuliko wote.
Hiyo inaitwa tamaa ya fisi! Anatazama angani na kuona mawingu meupe, akili yake inamwambia hiyo ama ni pamba, au nyama iliyojaa mafuta.
Ghafla anajiambia watu hawawezi kuhifadhi pamba juu hivyo kwa kuwa hakuna mnyama anayetaka kuila, lakini wanaweza kuangika nyama umbali huo ili fisi wasiifikie.
Anaketi hapo siku nzima, ila anaishia kunyeshewa tu, au kiza kinampata hapo akisubiri nyama ianguke, mwishowe anajiambia binadamu wamefunga duka la nyama.
Naambiwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapendekeza ipitishwe sheria itakayoipa mamlaka ya kukataa orodha za wabunge maalum wanaoteuliwa na vyama ikiwa hazitazingatia sheria inayosema jinsia moja isishikilie zaidi ya thuluthi mbili za nyadhifa za umma.
IEBC imelazimika kufanya hivyo eti kwa kuwa wanaume wasiposhurutishwa hawatawahi kutekeleza sheria hiyo, wataendelea kuvuta ngoma kwao.
Napendekeza wanaume wakatazwe kumchagua ‘mama kaunti’, wawaachie wanawake kazi hiyo. Mwanamume kamili unafanya nini katika uchaguzi ambapo wanawake wanamchagua mwakilishi wao?