Uvumbuzi: Mwanafunzi anayeunda vyungu vya miche kwa kutumia maganda ya mananasi
AKIWA na umri wa miaka 23 pekee, Maxwell Tom Oyoo, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kabianga, ameonyesha umahiri kwenye tasnia ya ubunifu inayolenga kuboresha sekta ya kilimo.
Anasomea Shahada ya Masuala ya Uchumi katika chuo hicho kilichoko Kericho, na hakujua kuwa video aliyotazama awali kwenye You-Tube ingeishia kuwa jukwaa la kutoa suluhu kwenye kilimo.
“Tulikuwa tumepewa kazi kutafiti mitandaoni na ni katika pilkapilka hizo nilikutana na video ya You-Tube jinsi taka za kilimo zinavyoweza kubadilishwa kuwa bidhaa muhimu,” anakumbuka.

Kilichoanza kama mradi wa darasani sasa kimekuwa uvumbuzi wa kiikolojia (eco system) – vifaa vya kupandia miche visivyo na madhara yoyote kwa mazingira.
Aidha, Tom sasa ni mbunifu anayeunda vyungu vya kukuzia mseto wa miche anavyotengeneza kutokana na maganda ya mananasi.
Akiwa katika kipindi cha lala salama chuoni, ni mwanafunzi mwanaharakati wa mazingira na mtetezi wa uhifadhi wa ikolojia.
“Nimekuwa nikitetea uhifadhi wa mazingira kila wakati,” anasema.
Kwa wengine maganda ya mananasi ni taka, lakini kwake ni dhahabu.

“Wengi huyatupa baada ya kula matunda, lakini mimi niliona fursa ya kuyatumia kutengeneza kitu chenye thamani na rafiki kwa mazingira,” anaelezea.
Mchakato huanza kwa kukusanya maganda kutoka masokoni. Baada ya hapo huyakausha, kuyakatakata kuwa vipande vidogo na kuvisaga kwa mashine.
Unga unaopatikana huchujwa, kisha unachanganywa na unga wa mahindi uliosheheni wanga (cornstarch) ambao hufanya kazi kama gundi asilia.
“Tunaunda mchanganyiko wenye mwonekano wa udongo, kisha tunauweka kwenye vifaa vyenye maumbo ya chungu,” anafafanua.

Chungu kidogo kilichofinyangwa – chenye kipenyo (diameter) cha sentimita sita huuza Sh50, na kile kikubwa cha kipenyo cha sentimita tisa Sh100.
Vifaa hivyo vinatumika kupandia miche ya nyanya, kabichi na mboga nyinginezo.
Faida yake kubwa ni kwamba havihitaji kuondolewa wakati wa kupanda, kama anavyoelezea Tom. “Unapanda chungu kizima ardhini, na baada ya karibu siku 21 kinayeyuka na kuwa mbolea.”
Tofauti na plastiki zinazoharibu na kuchafua mazingira, vyungu vya Tom ni vya asili na vinavyooza haraka na kabisa.
Kwenye mahojiano na Akilimali, mwanafunzi huyo wa mwaka wa mwisho – wa nne alisema ubunifu huo ni mchango wake katika vita na kampeni dhidi ya uharibifu wa mazingira hasa katika kipindi ambacho taifa na ulimwengu unaashiria kulemewa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Isitoshe, anasisitiza ni mojawapo ya mbinu kuhamasisha kilimohai na endelevu.

Hata hivyo, safari yake kufikia alipo anakiri haijakuwa rahisi. “Majaribio ya kwanza yalishindikana; vifaa vilikuwa vikipasuka vilipopelekwa juani kukauka,” anasema.
Baada ya wiki tatu za majaribio, alifanikiwa kupata suluhu sahihi – uwiano kati ya wanga na maganda.
Sasa vyungu hivyo ni imara na vinadumu hadi miche inapohamishiwa shambani.
Tom anasema wazo hilo ni sehemu ya utafiti wake wa mwaka wa mwisho chuoni, analosema pia limepigwa jeki na wahadhiri wake kutokana na uvumbuzi wake wa kipekee.
Ingawa anasomea Shahada ya Masuala ya Uchumi, ni mkulima mdogo nyumbani kwao ambapo anadokeza kwamba hufanyia majaribio ya ubunifu huo.
“Nina kipande cha shamba nilichopewa na wazazi wangu ambapo huendeleza kutafiti kuboresha vyungu maalum ninavyounda.”

Ukakamavu wake, anasema umehamasisha vijana wenzake kutazama kilimo kama biashara.
Kando na vyungu vya miche, yeye na wanafunzi wenza hutengeneza bidhaa zingine kama jemu ya mkate, juisi na sharubati kwa kutumia sehemu tofauti za nanasi.
Chuo Kikuu cha Kabianga kilikuwa kati ya walioalikwa kushiriki Maonyesho ya Makala ya Tano ya National Agribusiness Summit, yaliyoandaliwa na Mtandao wa Washirika wa Kilimo Nchini, ndio Agriculture Sector Network (ASNET) kwa ushirikiana na Wizara ya Kilimo kati ya Oktoba 22 na 23, Ukumbi wa KICC, Nairobi.
Maonyesho hayo yenye kaulimbiu, “Kutoka Ahadi hadi Hatua: Kukuza Biashara ya Kilimo kupitia Majadiliano na Ubunifu”, yalidhuriwa na Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe aliyehimiza umuhimu wa teknolojia na ubunifu kuboresha shughuli za uzalishaji chakula nchini.
Tom, ana imani kuwa baada ya kufuzu chuoni atazamia uvumbuzi wake kikamilifu kufanikisha sekta ya kilimo.
