Akili MaliMakala

Ng’ombe wa maziwa ambaye mkulima amekataa kumuuza Sh10 milioni

Na SAMMY WAWERU December 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 4

NG’OMBE aina ya Friesian Holstein aliyeibuka bingwa mkuu (Supreme Champion) katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nairobi (Nairobi International Trade Fair) mwaka huu yaliyoandaliwa na Baraza la Kilimo Nchini (ASK), hulishwa wakati anapotaka kula.

Ng’ombe huyo wa maziwa mwenye uzito wa kilo 503 anayemilikiwa na Tassells Farm Ltd, Naivasha, mwasisi wa mradi huo Muturi Njoroge anasema siri iliyomuwezesha kuwahi tuzo ya ASK Nairobi 2025 kitengo cha ng’ombe wa maziwa ni kumtunza mithili ya yai.

“Humlisha wakati anapotaka kula, iwe asubuhi, mchana au hata jioni.”

Muturi Njoroge, Tassels Farms Ltd. Picha|Sammy waweru

Kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali, Muturi amedokeza kwamba amekumbatia mfumo wa mgao – ration, kuwapa ng’ombe wake malisho yaliyoafikia ubora wa chakula cha mifugo.

“Muhimu zaidi ni chakula unacholisha mifugo wako. Niko makini sana haswa kwa silage,” akaelezea.

Kwa siku, akikadiria Friesian Holstein aliyetazwa ushindi katika Makala ya 123 ya ASK, katika uwanja wa Jamhuri, mfugaji huyo alisema hula wastani wa kilo 50 hadi 60.

Anatokana na bridi aliyezalishwa kwa miaka mingi ili kupata yule bora, Muturi akisisitiza kwamba kuwapa ng’ombe chakula bora na faafu huondolea mifugo kero ya maradhi kama Homa ya Maziwa, Foot and Mouth Disease, Mastitis, kati ya mengineyo.

Ngombe wa Njoroge Muturi aliyepata tuzo bora zaidi kwenye maonyesho ya ASK Nairobi 2025. Picha|Sammy Waweru

“Malisho, mradi wetu hujikuzia. Mwanzo, huanza kwa kupima hadhi ya udongo ambayo huamua ubora wa chakula – silage,” akafafanua, akisisitiza sharti mavuno yafanywe wakati ufaao na kulisha mifugo vyema.

Ng’ombe bingwa mkuu aliyetawazwa taji ASK 2025, ni mkubwa na mwenye madoa meusi na meupe, uso mrefu, masikio yaliyonyooka na mgongo ulionyooka, alishangaza waliohudhuria.

Muturi alitabasamu kwa fahari wakati akikabidhiwa tuzo.

Lakini kilichoshangaza wengi si tuzo, bali ni kukataa kwake ofa kubwa ya kumuuza.

Je, angekubali kumuuza kwa Sh2 milioni?

“Siwezi kumuuza kwa ofa hiyo. Hiyo ni bei ya chini sana ikilinganishwa na thamani yake halisi. Kwa nini nimuuze sasa ilhali ng’ombe huyu anaweza kunizalia ndama watakaoniletea mapato makubwa kuliko hayo?” aliuliza Muturi.

Njoroge Muturi anadokeza kuwa ng’ombe aliyetuzwa ASK Nairobi 2025 huzalisha wastani wa lita 56 za maziwa kwa siku. Picha|Sammy Waweru

Alipoulizwa kama ofa ya Sh10 milioni ingetosha kumshawishi, Muturi alijibu kwa uthabithi: “Hata nikipewa Sh10 milioni kwa ng’ombe huyu bingwa ASK 2025, kamwe siwezi kumuuza. Nataka kuacha urithi kwenye mradi wangu kwa kuzalisha ng’ombe watakaokuwa bora zaidi kuliko huyu.”

Ni kauli inayowekwa muhuri na Simon Wagura, mtaalamu wa masuala ya mifugo, akisema aghalabu ng’ombe wa maziwa huwa ghali.

“Ng’ombe aina ya Friesian (mwenye umri zaidi ya miaka miwili) anayezalisha maziwa, bei yake haipungui Sh130, 000. Ni muhimu mkulima pia kuwa na bima yake,” anaelezea mtaalamu huyo.

Muturi alifichua kuwa ng’ombe aliyetunukiwa ameandikishwa rasmi kwenye nakala ya Kenya Stud Book na ana kitambulisho cha kitaifa cha mifugo, baada ya kuthibitishwa kuwa bridi bora na mama wakati wa kujifungua. Hii ina maana kuwa Friesian Holstein huyo amethibitishwa kuwa bora zaidi na kituo cha jenetiki za mifugo, kwa Kiingereza ndiyo Kenya Animal Genetic Resources Centre (KAGRC) tangu akiwa ndama, hivyo kumpa mfugaji haki ya kuweka bei yoyote ile anayotaka.

Akiwa na uzito wa kilo 503, ameshinda tuzo kadhaa kwenye makala ya maonyesho ya ASK hapo awali akiwa mdogo kabla ya kuzaa.

“Amezalisha ndama bora zaidi na wenye uzito, bila ulemavu, makosa ya kijenetiki au maradhi. Ana uzao wa hali ya juu kabisa,” Muturi ambaye aliingilia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa 2004 aliambia Akilimali.

Mojawapo wa ng’ombe wa Njoroge Muturi akitoa maziwa kwenye chuchu wakati wa maonyesho ya ASK Nairobi 2025, Jahmuri Grounds. Picha|Sammy Waweru

Katika maonyesho ya ASK Nairobi 2025, jopo la majaji huru lilimtawaza ng’ombe huyo kuwa bingwa mkuu baada ya kutimiza vigezo vyote vya ng’ombe bora wa maziwa — kwa kuwa na mwili ulio imara, uwezo wake wa kutoa maziwa mengi, maumbile mazuri, kukosa magonjwa, na mwenye afya bora na kuzalisha kiwango ncha juu cha maziwa.

Muturi alikuwa na ng’ombe washindani watatu, lakini ng’ombe wake huyo mwenye umri wa miaka mitano aliibuka kidedea na kutambuliwa kama ng’ombe wa hadhi ya juu zaidi katika uzalishaji wa maziwa.

Kaulimbiu ya maonyesho ya mwaka huu ilikuwa “Promoting Climate-Smart Agriculture and Trade Initiatives for Sustainable Economic Growth,” na kupitia Makala hayo ya 123 ya ASK Muturi alitambuliwa kuwa mfugaji bora zaidi wa ng’ombe wa maziwa Kenya.

Maonyesho hayo yalifunguliwa rasmi na Rais William Ruto mnamo Septemba 29, na kukamilika Jumapili, Oktoba 5, 2025.

Ngombe wa Njoroge Muturi aliyepata tuzo bora zaidi kwenye maonyesho ya ASK Nairobi 2025. Picha|Sammy Waweru

Muturi anadokeza kuwa ng’ombe wake huzalisha wastani wa lita 56 za maziwa kwa siku.

“Kwa sasa ndiye anazalisha maziwa mengi zaidi. Tuzo hii ni heshima kubwa kwa mfugaji yeyote yule, kwa sababu inathibitisha kisayansi ubora wa kizazi chake,” alisema kwa fahari.

Akiwa na Shahada ya Masuala ya Afya ya Wanyama kutoka Israili, Muturi anasema amejifunza mengi kutoka kwa sekta ya maziwa ya nchi hiyo.

“Kile kinachowafanya Waisraili wawe bora ni jinsi wanavyoshughulikia mifugo wao. Hawasubiri ng’ombe waugue; wanachukua tahadhari mapema – kulisha vizuri, kuwapa chanjo, matibabu, kudumisha kiwango cha usafi na ufuatiliaji wa afya,” alifafanua.

Ni vigezo ambayo Muturi huwa makini navyo, kwa siku akikadiria ng’ombe wake hunywa karibu lita 80 za maji. “Ng’ombe unavyompa chakula cha kutosha na maji, ndivyo hukupa maziwa mengi.

Kiwango cha usafi kwenye zizi nacho ni cha hali ya juu, wanyama wake wakilalia magodoro yaliyotandazwa eneo tambarare.

Ng’ombe wa Muturi Njoroge alitawazwa kuwa Supreme Champion, ishara kuwa ndiye bora zaidi Kenya katika uzalishaji maziwa. Picha|Sammy Waweru

Anasema ana mtaalamu wa kila suala kuanzia malisho, vetinari, wa kilimo – uzalishaji wa silage, miongoni mwa wengine, akishirikiana kwa karibu na Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Safari yake ilianza na ng’ombe wanne pekee anaofichua kwamba aliwanunua kwa jumla ya Sh180, 000.

Leo hii, hata ingawa hakutaja idadi kamili ya ng’ombe anaomiliki, anasema mradi wake umekua mkubwa na kwa kasi.

“Mradi unaozalisha ng’ombe bingwa anayetawazwa Kenya nzima ni ishara kuwa si mdogo.”

Kwa sasa, Muturi huuza maziwa kwa Sh45 kwa kila lita, mengi ya maziwa yake yakisambazwa kupitia mtambo wa ATM maeneo mbalimbali nchini.

Safari yake kwenye ufugaji wa ng’ombe wa maziwa haijakuwa mteremko. Anakumbuka miaka kadha iliyopita alipopoteza ng’ombe wapatao 18 kupitia maradhi ya East Coast Fever (ECF).

Mfugaji Muturi Njoroge anamiliki Tassels Farm, mradi anaosema una ng’ombe wengi wa maziwa. Picha|Sammy Waweru