Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mirathi ya mwanamke wa Kiislamu kwa mujibu wa Qur’an na Sunnah

February 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na neema ndogondogo.

Tumejaaliwa leo hii kukutana katika ukumbi huu wetu wa kuangazia maswala muhimu yanayoihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote twachukua nafasi hii adhimu na adimu kumshukuru mno Mola wetu Mkuu kwa kuwa ni yeye pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa.

Ni Yeye pekee ndiye mwenye heshima, utukufu na ndiye Muumba wa ardhi, mbingu na vyote (viumbe) vilivyomo.

Aidha, katika uzi uo huo twachukua nafasi hii kumtilia dua na kumtakia kila la kheri Mtume wetu (SAW).

Mada ya leo ndugu zangu waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu imetokana na maamuzi ya majuzi ambapo mahakama moja nchini iliamua kuhusu haki ya wanawake kupata haki yao kwa maana ya mirathi. Mdahalo huo ungalipo katika makiwanda mbali mbali.

Wengi kutoka dini nyinginezo wanasherehekea (wanawake) wakidai kuwa walikuwa wametelekezwa na kubaguliwa.

Kinachosahaulika katika mjadala huo ni kuwa dini yetu tukufu ya Kiislamu imeweka wazi kila jambo, likiwemo swala hilo hilo la mirathi.

Kwa mujibu wa baadhi ya mifumo ya kisheria ya kale, mtoto wa kike alipata urithi lakini watoto wake hawakupata.

Kwa upande mwingine, mtoto wa kiume sio tu anapata urithi yeye mwenyewe, bali pia watoto wake walirithi mali iliyoachwa na mababu zao.

Baadhi ya mifumo mingine ya sheria ilimruhusu mwanamke kurithi lakini si kwa kupata asilimia maalum au kwa lugha ya Qur’ani ‘gawio lililopangwa.’

Walichokifanya ilikuwa ni kumruhusu mzazi kuusia kuwa apewe, kama muusiaji anataka.

Kuzuia mali kuhama

Sababu kuu ya kumnyima mwanamke urithi ilikuwa ni kuzuia kuhama kwa mali kutoka familia moja kwenda nyingine.

Kwa mujibu ya imani za kale, mchango wa mwanamke katika uzazi haukuwa wa thamani sana.

Akina mama walitumika kama mifuko tu ambamo mbegu ya baba ilikua na kuwa mtoto. Kwa sababu hii waliamini kuwa watoto wa mtoto wa kiume walikuwa sehemu ya familia lakini watoto wa mtoto wa kike hawakuwa sehemu ya familia yake, kwa vile walikuwa sehemu ya familia ya babu yao mzaa baba.

Hivyo kama binti angepata urithi, hiyo ingemaanisha kuhamisha mali kwenda kwa watoto wake (binti), watoto ambao hawahusiani na familia ya marehemu.

Kwa sababu hii, Waarabu wa zama za kabla ya Uislamu, walikuwa hawakubali suala la mwanamke kurithi mali, maadamu kulikuwepo wanafamilia wa kiume hata kama kiukoo walikuwa ni ndugu wa mbali.

Hii ndio sababu walishangazwa sana Qur’ani iliposema wazi wazi kuwa: “Wanaume wana sehemu katika kile kinachoachwa na wazazi na ndugu wa karibu, kiwe kikubwa au kidogo gawio lililopangwa.” (Suratul Nisa, 4:32).

Ilipata kutokea wakati fulani ndugu yake na Hasan bin Thabit, mshairi maarufu, alifariki katika siku hizo, huku akiacha mke na binti zake wengi.

Binamu zao wa mfumo dume waligawiana mali zote na hawakuwapa chochote mjane na binti zake.

Mjane alilalamika kwa Mtume ambaye aliwaita ndugu wa mume.

Walisema kuwa mwanamke hakuwa na uwezo wa kubeba silaha na kupigana na adui. Ni wanaume waliojilinda wao na wanawake.

Hivyo ni wao tu waliokuwa na haki ya kurithi mali.

Sheria ya mirathi ya Kiislamu imeepukana na mapungufu yote ya huko nyuma.

Kitu kinachopingwa na wale wanaodai kutetea usawa kati ya mwanaume na mwanamke, ni kwamba gawio la mwanamke ni nusu ya gawio la mwanaume.

Kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu mtoto wa kiume hupata mara mbili ya mtoto wa kike, kaka hupata mara mbili ya dada yake na mume hupata mara mbili ya kile anachopata mke wake.

Gawio la baba na mama ndio halifuati utaratibu huu.

Kwa sababu zilizotajwa hapo awali, Uislamu unachukulia matunzo na mahari kuwa ni mambo muhimu na ya lazima katika kuiimarisha ndoa. Yanatoa hakikisho la maelewano na masikilizano.

Ama kweli dini ya Uislamu haibagua jinsia, rangi wala kabila. Hata mwanamke amepewa hadhi yake,tena kubwa sana!

Ijumaa Kareem!
Baruapepe ya mwandishi: [email protected]