• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vipengele vinavyodhihirisha uhusiano kati ya Isimu na Isimujamii

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vipengele vinavyodhihirisha uhusiano kati ya Isimu na Isimujamii

Na MARY WANGARI

KWA mujibu wa Msanjila na wenzake (2011), katika mkabala wa mawanda mapana sababu za uteuzi wa lugha kuchukua dhima ya kitaifa, ama ukipenda kuwa lugha ya taifa, kuwa lugha rasmi au kuwa lugha ya kufundishia hazitokani na sababu za kiisimu pekee au kiisimujamii pekee bali hazina budi zitokane na sababu za pande zote mbili za kiisimu na kiisimujamii kupitia kigezo hiki ukamilishano huonekana dhahiri.

Isitoshe, Msanjila na wenzake (2011) wanasema kwamba, “kwa kusikiliza mazungumzo ya watu mbalimbali utagundua kuwa kuna vibainishi vya lugha ambavyo ni vya kisayansi (isimu) anavyovitumia mwanaisimujamii katika kubainisha aina ya watu wanaohusika katika mazungumzo kama ni wajamii fulani, mfano Wakisii, Wapokomo, Wakikuyu, iwapo ni wasomi au si wasomi na kadhalika” (Msanjila et al, 2011, uk.9).

Vibainishi hivyo vinaweza kuwa ni vya kifonoloja, kimofolojia, kileksika na kifonetiki.

Kwa mfano, wazungumzaji wengine hutamka /ch/ingine badala ya /k/ingine, /n/tu badala ya /m/tu au ‘thatha’ badala ya sasa.

Hivyo basi, mwanaisimujamii habaini haya endapo tu ataihusisha taaluma ya isimu.

Besha (2007) anasema, “lengo la isimu si kuwafundisha watu jinsi ya kuzungumza lugha yao, yaani kipi waseme na kipi waache. Bali lengo la isimu ni kuweka wazi kanuni zinazotawala lugha ambazo wazungumzaji wanazitumia bila wao wenyewe kuzijua” (Besha, 2007, uk.10).

Hivyo katika kuweka kanuni hizo jambo la msingi awali ya yote ni lazima isimu ijue ni namna gani lugha inatumika katika jamii.

Kutokana na hoja hii inajidhihirisha wazi kuwa isimu itategemea matokeo ya utafiti wa isimujamii kuhusu matumizi ya lugha katika jamii ndipo iweze kuweka kanuni hizo.

Hivyo basi, isimu na isimujamii ni taaluma mbili zinazokamilishana.

Isimu na isimujamii haviwezi kutenganisha kwani taaluma zote hizi mbili hutegemeana na hukamilisha.

Ili isimu ikamilishe malengo yake, hutumia isimujamii kwani katika jamii ndimo lugha hutumika.

Vilevile isimujamii haiwezi kubaini tofauti za uzungumzaji katika jamii pasipo kuihusisha isimu ambayo ndiyo sayansi ya lugha.

Kwa mtazamo huu, isimu na isimujamii huweza kuonekana kama pande mbili za sarafu moja zilizo na picha mbili tofauti katika kila upande, ambazo kimsingi hukamilishana na kuipa thamani sarafu hiyo.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia. Dar es Salaam: BAKITA.

Mulokozi, M. M. (1991) “English versus Kiswahili ni Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studies Ghent.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mirathi ya mwanamke wa Kiislamu kwa...

Aduda alia mashabiki hawafiki uwanjani

adminleo