Michezo

Bradley ibs ndiye kocha bora wa SJAK Novemba

Na CECIL ODONGO December 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MKUFUNZI wa Nairobi City Thunder, Bradley Ibs, ametajwa kuwa Kocha Bora wa Mwezi wa Novemba wa tuzo ya Chama cha Wanahabari wa Michezo nchini Kenya (SJAK) inayodhaminiwa na kampuni ya Betika.

Mwezi Novemba, Mwamerika huyo aliiongoza Nairobi City Thunder kufuzu kwa mara ya pili mfululizo kwa Ligi ya Afrika ya Mpira wa Vikapu ya Wanaume (BAL) mwaka 2026.

Mbele ya umati mkubwa wa mashabiki katika Ukumbi wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi, City Thunder iliandikisha historia baada ya kufunga Ferroviario da Beira ya Msumbiji kwa alama 109-70 katika fainali ya Road to BAL Elite 16 (East), na hivyo kujihakikishia nafasi yao katika mashindano ya BAL.

Mabingwa hao wa Kenya, wakiongozwa na Ibs na waliocheza kwa mara ya kwanza katika BAL mwaka jana, walifanikiwa kupata tena mafanikio hayo kwa kufuzu wakiwa nyumbani. Walikuwa timu ya kwanza katika Elite 16 ya mwaka huu kufikisha alama 100 katika mchezo mmoja.

Kuibuka bora mwezi Novemba, Ibs alishinda wagombea wengi wenye ushindani mkali, akiwemo kocha wa Kenya Police FC Bullets, David Vijago, ambaye timu yake haikupoteza mechi, pamoja na Kevin Wambua wa Kenya Morans aliyeongoza timu ya Kenya Sevens kushinda bila kupoteza katika mashindano ya Zambezi Sevens nchini Zimbabwe.

Ibs alionekana mwenye furaha kubwa alipokabidhiwa tuzo hiyo:
“Nimefurahi sana kupokea tuzo hii,” alisema Ibs.

“Ninajivunia kazi ngumu na kujitolea kwa timu yangu. Tunafurahia fursa ya kuiwakilisha Kenya tena katika jukwaa la bara.”