Habari

Hatutakabidhi Amerika data binafsi za Wakenya, Serikali yajitetea

Na SAM KIPLAGAT December 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imejitokeza kuwaondolea wananchi hofu ya data muhimu za kibinafsi kuhamishwa Amerika kufuatia mkataba wa ushirikiano wa afya wa mabilioni ya pesa uliotiwa saini jijini Washington mapema mwezi huu.

Katika ombi lililowasilishwa katika Mahakama Kuu kuomba kuondolewa kwa maagizo yanayozuia utekelezaji wa makubaliano hayo, Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, alifafanua kuwa Kenya haitafichua data yoyote nyeti ya kibinafsi ya raia wake.

Mwanasheria Mkuu alisisitiza kuwa data itakayotolewa ni ya jumla tu isiyomtambulisha mtu yeyote, na itatumika mahsusi kutekeleza Mfumo wa Ushirikiano.

“Ni muhimu kubainisha kuwa, kama inavyoelezwa wazi chini ya Makubaliano ya kubadilishana Data, Serikali ya Kenya haitatoa data yoyote muhimu ya kibinafsi ya raia wake, bali itatoa data ya jumla pekee kwa madhumuni ya utekelezaji wa Mfumo wa Ushirikiano,” ilisema serikali katika maombi hayo.

Mahakama Kuu ilisimamisha utekelezaji wa Mfumo wa Ushirikiano wa Afya wa miaka mitano, ikisubiri uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na Shirikisho la Watumiaji Kenya (Cofek), lililoeleza hofu ya ukiukaji wa data za matibabu.

Shirikisho hilo lilidai kuwa mara data za matibabu za Kenya zitakapohamishwa nje ya nchi, madhara yatakuwa ya kudumu na yasiyoweza kurekebishwa.

Cofek iliongeza kuwa mahakama au wasimamizi wa sheria wa Kenya hawatakuwa na mamlaka ya kurejesha, kudhibiti au kusimamia matumizi ya data hizo nje ya nchi mara zitakapotolewa chini ya makubaliano kati ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo, serikali iliomba mahakama iondoe amri hiyo ikisema kuwa kufanya hivyo hakutasababisha madhara yasiyorekebika, kama inavyodaiwa, ikizingatiwa kuwa utekelezaji wa mfumo huo hauhusishi kutolewa kwa taarifa zinazomtambulisha mtu binafsi.

Ombi hilo liliongeza kuwa kutolewa kwa data, kama inavyopendekezwa chini ya mfumo huo, kunahusisha data ya jumla pekee.

Serikali ilifafanua kuwa data ya jumla ni data iliyofupishwa na isiyomtambulisha mtu, inayotumiwa kwa ufuatiliaji na tathmini, utoaji wa taarifa kwa umma na upangaji mipango.