Uhuru asifu ujasiri wa Gen Z, awahimiza wapiganie uongozi
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amewahimiza vijana wa Afrika kujitokeza na kuchukua nafasi za uongozi sasa, akionya kuwa wale wanaosubiri siku zijazo wapewe madaraka wako hatarini kukosa fursa yao.
Akizungumza jana katika Mkutano wa Mwaka wa Wahitimu wa Chuo cha Uongozi cha IGAD (IGAD Leadership Academy – ILA) uliofanyika katika Hoteli ya Windsor, Nairobi, Bw Kenyatta aliwaambia washiriki kuwa dhana ya “viongozi wa kesho” ni potofu, na kuwataka vijana wachukue hatua kwa ujasiri katika kuunda hatima ya Afrika.
“Ikiwa mtaendelea kuamini kuwa ninyi ni viongozi wa kesho, basi hiyo kesho haitawahi kufika,” alisema. “Ninyi ni viongozi wa leo. Mawazo yenu, ujasiri wenu na kujitolea kwenu binafsi ndivyo vitakavyoamua mustakabali wa Afrika.”
Rais huyo wa zamani aliwakumbusha vijana kuwa viongozi wa awali wa Kenya akiwemo Tom Mboya na Kenneth Matiba walianza kuunda mwelekeo wa taifa wakiwa na umri wa miaka ya ishirini, akisisitiza kuwa ujana si kikwazo cha kuleta mabadiliko makubwa.
Mkutano huo uliokuwa na kaulimbiu ‘Kuimarisha uongozi wa vijana ili kuchochea ukuaji wa Afrika’ uliwaleta pamoja wahitimu wa Chuo cha Uongozi cha IGAD, wanachama wa mabalozi na viongozi wa kikanda, akiwemo Katibu Mkuu wa IGAD, Dkt Workneh Gebeyehu, Seneta Crystal Asige miongoni mwa wageni wengine mashuhuri, kusherehekea kizazi kipya cha uongozi wa Afrika chenye maadili na ushirikiano.
Katika hotuba yake kuu, Bw Kenyatta aliwasifu vijana kote katika kanda kwa kuchukua hatua katika masuala ya kijamii na kibinadamu, akisema umoja wao ni ushahidi kuwa ufufuo wa Afrika tayari umeanza. Alitaja mkutano huo kama “harakati ya viongozi vijana waliojitolea kubadilisha bara.”
Kwa upande wake, Dkt Workneh alisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa vijana kama msingi wa amani ya kudumu na umoja wa kikanda. Alisema changamoto zinazokabili Pembe ya Afrika hazisababishwi na hatima bali na maamuzi ya binadamu, na kwamba kizazi kijacho lazima kiandaliwe kufanya maamuzi bora zaidi.
“Iwapo tunataka kufikia ushirikiano wa kweli wa kikanda, lazima kwanza tuukuze uwezo wa akili za vijana,” alisema Dkt Workneh. “Hatima zao zimeunganishwa, na mustakabali wa eneo letu unategemea jinsi watakavyojifunza kufanya kazi pamoja kuanzia leo.”
Seneta Crystal Asige aliwataka viongozi vijana kushughulikia uongozi kwa kina, kusudi na misingi ya kiroho. Aliwahimiza kufikia ubora usioweza kupuuzwa, akiwakumbusha kuwa mafanikio ya kweli huanzia na unyenyekevu na bidii.
Wazungumzaji wengine katika hafla hiyo walikuwa pamoja na Bi Riina-Riikka Heikka, Balozi wa Finland nchini Kenya, na Tomonobu Hori, Naibu Balozi wa Japani nchini Kenya.