Mjane, mtoto wa miaka 7 waomba fidia ya Sh700M kwa kifo cha mume, baba
MVULANA ambaye baba yake aliuawa na polisi miaka minane akishirikiana na mama yake ameishtaki serikali akiomba korti imfidie Sh700milioni.
Mvulana huyo mwenye umri wa miaka saba aliambia mahakama kuu ya Milimani kupitia wakili mwenye tajriba ya juu Ahmednassir Abdullahi kwamba “kitendo cha polisi kumuua baba yake bila hatia kilimpokonya mwelekezi na mshauri maishani.”
Mahakama ilielezwa kwamba Katiba ya Kenya imempa kila raia uhuru wa kuishi na kuitaka serikali iyalinde maisha ya kila mtu bila kuzingatia rangi , kabila na uraia.
“Naomba hii mahakama iamuru serikali imlipe mvulana huyu kima cha Sh18milioni hii ikiwa ni Sh1milioni moja kila mwaka hadi atakapotimu miaka 18,” Bw Abdullahi alimweleza Jaji Enock Chacha Mwita anayeisikiza kesi hiyo ya kumfidia mjane huyo na mwanawe.
Mahakama ilielezwa kwamba serikali ya Kenya imekuwa ikiwaua wananchi wake na kukaidi vipengee vya katiba kwamba imejukumizwa kuyalinda maisha na mali ya wananchi.
Mahakama ilifahamishwa kwamba Kifungu nambari 53 cha Katiba ya Kenya kimeeleza kwamba kila mtotot “yuko na haki ya kuwa na wazazi wanataojitahidi kumlea , kumlinda, kumuelimisha na kumtunza.”
Mahakama ilijulishwa na wakili kwamba mnamo usiku wa Oktoba 17 2017 polisi waliyavamia makazi ya Bunty Bharati Kumar Shah na kumpiga risasi kifuani akafa papo hapo.
Bunty ambaye pia anajulikana kwa jina Bunty Bobby Shah alikuwa mkurugenzi katika kampuni ya kutengeneza magodoro ya Bobby Mills Limited.
Alikuwa anapokea mshahara wa Sh600,000 na marupurupu ya Sh500,000 kila mwisho wa mwaka.
Mahakama ilijuzwa kwamba polisi wasiopungua 30 wakiwa wameabiri magari kadhaa walivunja lango la makazi ya Bunty na kuingia mle.
Alikuwa na umri wa miaka 32 alipotandikwa risasi kifuani.
“Marehemu alisikia kelele nje ya makazi yake na alipovuta kateni ya dirisha polisi walimchapa risasi kifuani.Alikufa papo hapo. Alikuwa na mkewe na mtoto wao mwenye umri wa miezi mitano ambaye sasa yuko na umri wa miaka saba (7),” jaji alielezwa na wakili.
Tangu wakati huo, mtoto alimpoteza baba yake na mkewe akampoteza mume.
Wakili alieleza mahakama kwamba Katiba ya nchi hii imevitaka vyombo vya usalama vya nchi hii kulinda maisha na mali na “wala sio kuyatwaa.”
Akionyesha makasiriko Bw Abdullahi alimweleza Jaji Mwita , “Tangu nchi hii ijinyakulie uhuru wake serikali zote zimekuwa zikiwaua watu wasio na hatia. Naomba hii mahakama iamuru serikali ifidie familia ya marehemu aliyekuwa mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza magodoro zaidi ya Sh700milioni ipate funzo na ianze kuyathamini kuyalinda na kuyatunza maisha ya watu,” wakili alimrai jaji huyo.
Wakili huyo alieleza korti kwamba maisha ya kila mwananchi ni muhimu sana na kamwe “hayapasi kutwaliwa na polisi kiholela.”
Bi Anjlee Parveen Kumar Sharma, mjane wa Bunty amewashtaki Mwanasheria Mkuu (AG), Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) na Waziri wa Usalama kwa mauaji hayo.
Mjane huyo aliomba mahakama itangaze kuangamizwa kwa mumewe na kitengo cha uslama cha serikali ni ukiukaji wa haki zake na mtoto wao-ambaye sasa hana baba wa kumwongoza na kumshuari.
AG kupitia kwa wakili wa serikali alipinga fidia hiyo akisema haiwezekani kulipwa.
AG alisema kwamba majina katika kitambulisho na yale yako kwa kesi hayafanani.
Mahakama ilielezwa na mjane huyo kwamba hawasilisha ushahidi wa kutosha kudhibitisha anastahili kulipwa fidia hiyo.
Uamuzi wa kesi hiyo utatolewa Machi 20,2026.