Pigo kwa Ligi Kuu ya Uingereza AFCON ikiwadia
RABAT, MOROCCO
FAINALI za Kombe la Afrika (AFCON) zinaanza Jumapili 21 hadi Januari 18, huku klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zikiathirika pakubwa kwani zitawakosa wachezaji wao muhimu watakaochezea timu zao za taifa wakati wa fainali hizo za bara.
Kulingana na ratiba ya michuano hiyo itakayofanyika nchini Morocco, wachezaji hao watakosa hadi mechi sita za EPL- pamoja na nyingine za FA Cup na Carabao.
Kwenye mechi ya ufunguzi, wenyeji Morocco wamepangiwa kucheza na Comoros katika uwanja wa Stade Prince Moulay Abdalla jijini hapa.
Miongoni mwa timu zilizoathirika zaidi ni Sunderland, Manchester United, Fulham na Burnley.
Sunderland itapoteza wachezaji sita wanaojumuisha Noah Sadiki wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) pamoja na raia mwenzake Arthur Masuaku, Reinildo Mandava (Msumbiji), Bertrand Traore (Burkina Faso), Chemsdine Talbi (Morocco) na Habib Diarra (Senegal).
Manchester United watapoteza wachezaji watatu ambao ni Brian Mbeumo (Cameroon), Amad Diallo (Ivory Coast) na Noussair Mazraoui (Morocco).
Burnley italazimika kucheza bila Axel Tuanzebe (DRC), Lyle Foster (Afrika Kusini) na Hannibal Mejbri (Tunisia) huku Fulham ikiwapeza Wanigeria Alex Iwobi, Samuel Chukwueze na Calvin Bassey.
Manchester City, Tottenham Hostpur, Everton, Brentford na Nottingham Forest watasakata kabumbu kwa majuma manne bila wachezaji wawili wawili kwa kila timu.
Omar Marmoush (Misri) na Rayan Ait-Nouri (Algeria) wanaondoka mikononi mwa kocha Pep Guardiola kufanyia timu zao vibarua.
Mali imemjumuisha kikosini Yves Bissouma huku Pape Matar Sarr akiitwa na Senegal tayari kwa AFCON hivyo basi kuinyima Spurs vifaa muhimu.
West Ham ambayo imewaachilia Aaron Wan-Bissaka (DRC) na El Hadji Malick Diouf (Senegal), pamoja na Wolves zitawakosa wachezaji wawili wawili pia.
Liverpool itacheza majuma hayo manne bila Mohamed Salah wa Misri.
Kuelekea fainali hizo, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limechapisha orodha ya vitu ambavyo vimepigwa marufuku ndani ya viwanja kwa lengo la kuhakikishia kila mtu salama wake.
Miongoni mwa vitu hivyo ni silaha, fataki, vifaa vinavyoweza kuwaka, filimbi za kupuliza, tarumbeta, pembe za wanyama, miavuli kubwa na helmeti.
Kadhalika pombe, dawa za kulevya, sigara pamoja na mabango ya kisiasa vimepigwa marufuku.