Habari

Krismasi: Kampuni yazindua kampeni ya Sh30m ‘Fizzmas’ Wakenya wakijiandaa kwa sikukuu

Na WINNIE ONYANDO December 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WENGI husafiri kujumuika na familia msimu huu wa Sikukuu.

Wakati huu pia ni wa kusherehekea na familia na marafiki na kwa msingi huu, kampuni ya vinywaji ya Pepsi, kupitia SBC Kenya, imezindua kampeni ya thamani ya Sh30 milioni almaarufu Fizzmas, ikilenga kuongeza uwepo wa bidhaa zake katika maeneo ya umma wakati wa msimu wa sikukuu.

Kampeni hiyo itatekelezwa kuanzia Desemba hadi mapema Januari, kipindi ambacho hushuhudia ongezeko la safari, ununuzi na shughuli za kijamii.

Fizzmas itafanyika katika maduka makubwa, kumbi za burudani, vituo vya mafuta na mikahawa kote nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Meneja wa SBC Kenya, John K’Otieno, alisema mkakati wa kampeni umejikita katika uwepo wa chapa badala ya kuwahusisha wateja katika michakato ya promosheni.

“Fizzmas inalenga kuwafikia Wakenya walipo; katika tamasha, maduka makubwa, barabarani na katika maeneo ya kijamii,” alisema K’Otieno, akiongeza kuwa msimu wa sikukuu ni wa kushirikiana na kufurahia pamoja.

Kampuni hiyo pia imeshirikiana na migahawa na vituo vya chakula ili kupanua kampeni hiyo kitaifa, huku ikilenga wasafiri wa sikukuu kupitia vituo vya mafuta vilivyo katika barabara kuu.

Kwa mtazamo wa biashara, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa SBC Kenya, Martin Kariuki, alisema msimu wa sikukuu hutoa fursa ya kufikia wateja wapya.

“Fizzmas inatupa nafasi ya kuwafikia wateja katika jamii mbalimbali, barabarani, kwenye hafla na katika migahawa,” alisema Kariuki.