Epuka tembe hatari, jaribu vyakula hivi kusisimua nguvu za kiume
TAFITI zinaendelea kuonyesha kuwa wanaume wengi wanakumbwa na tatizo la nguvu za kiume, huku mtindo wa maisha ukionekana kuchangia shida hii.
Ni suala ambalo limewasukuma wengi kuanza kutumia tembe za kuongeza nguvu hii, suala ambalo linazidi kuhatarisha maisha ya wengi.
Hata hivyo, kuna vyakula, ambavyo kulingana na wataalam, mtu akivizingatia, vinaweza kusaidia katika harakati hizo.
Unashauriwa kula vyakula vya baharini angaa mara mbili kwa wiki. Samaki wa mafuta wana manufaa mwilini kutokana na sababu kuwa wana viwango vya juu vya asidi za mafuta za omega-3.
Aidha, waweza kuongeza viwango vya asidi za mafuta mwilini kwa kunywa mafuta ya samaki au kwa kutumia vijalizo vya omega-3.
Mboga kama vile spinachi na sukuma wiki zina viwango vya juu vya madini ya magnesium, ambayo imethibitishwa kuimarisha viwango vya homoni za testosterone mwilini kwa wanaume.
Vyakula vingine vilivyo na viwango vya juu vya madini haya ni maharagwe, pojo, kokwa, mbegu na nafaka ambazo hazijakobolewa.
Utafiti unaonyesha kwamba tangawizi ina uwezo wa kuongeza viwango vya homoni za testosterone, vile vile kuimarisha uwezo wa mwanamume kutungisha mimba.
Utafiti uliofanywa mwaka wa 2012 ulionyesha kwamba kutumia kiungo hiki kila siku kwa miezi mitatu kuliongeza viwango vya testerone kwa asilimai 17.7 miongoni mwa wanaume zaidi ya miaka 75, walioshiriki kwenye utafiti huo.
Vitunguu vina manufaa mengi ya kiafya ikiwa ni pamoja na kuthibitisha nguvu za moyo na kupunguza uzani.
Mbali na hayo, chakula hiki ni chanzo murwa cha virutubisho kadhaa na kemikali za kuondoa uchafu mwilini, sifa zinazoimarisha viwango vya homoni za testerone mwilini.
Tunda la komamanga lina viwango vya juu vya kemikali za kuondoa uchafu mwilini, ambazo husaidia kuimarisha afya ya moyo, vile vile kupunguza msongo wa mawazo.
Utafiti unaonyesha kwamba kunywa juisi halisi ya komamanga huongeza uwezo wa kuimarisha viwango vya homoni hizi mwilini.
Lakini hata unapojikakamua kuongeza nguvu za kiume kupitia mbinu hizi, unashauriwa kuepuka vyakula vinavyohifadhiwa kwa kemikali, pombe na sigara.