Michezo

Maskini Juventus kona mbaya baada ya kichapo cha Atletico

February 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

KAMPENI ya Cristiano Ronaldo na klabu yake ya Juventus kwenye ngarambe ya Klabu Bingwa Ulaya ilipata pigo Jumatano pale ilipobwagwa 2-0 na Atletico Madrid katika mechi ya mkondo wa kwanza uwanjani Wanda Metropolitano.

Ronaldo alirejea katika jiji hilo la Uhispania alikopata ufanisi mkubwa akisakatia Real Madrid, lakini ni mahasimu wake wa zamani waliokuwa wakisherehekea kipenga cha mwisho kilipopulizwa baada ya kuona lango kupitia kwa Jose Gimenez na Diego Godin.

Fowadi wa Juventus Cristiano Ronaldo audhibiti mpira awamu ya 16-bora Klabu Bingwa Ulaya Juve ilipokaribishwa na Club Atletico de Madrid uwanjani Wanda Metropolitan, Madrid mnamo Februari 20, 2019. Picha/ AFP


“Bado hatujakamilisha kazi,” alisema kocha wa Atletico, Diego Simeone. “Kuna mechi ya mkondo wa pili na tunajua kitakuwa kibarua kigumu.”

“Kwa bahati nzuri, hatukukubali kufungwa bao la tatu,” alisema kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri.

“Kwa sababu matokeo ya 2-0 yanaweza kubadilishwa. Bado hatujaaga mashindano.”

Hata hivyo, ushindi huu ndio ambao vijana wa Simeone walistahili kuupata. Antoine Griezmann alikuwa amegonga mwamba, huku teknolojia ya video (VAR) ikinyima Atletico bao mara mbili baada ya uamuzi wake mzuri kufutilia mbali penalti ya Diego Costa na kichwa cha Alvaro Morata kabla ya Gimenez kutikisa nyavu.

Huku Juventus ikijaribu kupigania sare ya kutofungana, Atletico ilionyesha ujasiri. Simeone alimwingiza uwanjani Morata, Thomas Lemar na Angel Correa, wote karibu baada ya dakika ya 60, na ni ujasiri huu uliozalisha matunda.
Juve bila shaka haijabanduliwa kutoka kipute hiki, hasa kwa sababu Costa na Thomas Partey wote watakosa mechi ya marudiano mjini Turin wakitumikia marufuku baada ya kula kadi za njano.

Hata hivyo, kukosa kupata bao la ugenini na kuzidiwa maarifa katika kipindi cha pili si dalili nzuri kwa Juve kupata ufufuo.

“Hawakupi nafasi,” alisema Allegri. “Wanakufanya unacheza vibaya.”

Timu zote zitaingia mechi ya marudiano na presha ya kusonga mbele. Atletico, ambayo uwanja huo wake wa nyumbani utatumika kwa fainali ya Klabu Bingwa mnamo Juni 1 itapata fursa nzuri ya kupokonya Real taji katika mji huu ambapo zinatoka.

Nayo Juventus, ambayo imesubiri taji hili la kifahari kwa miaka 23, imekuwa na matarajio makubwa kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake tangu mchana-nyavu matata Ronaldo awasili.