Habari

Ajira kupungua mwanzo wa 2026- utafiti

December 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKUU wa mashirika ya sekta ya binafsi wanajiandaa kupunguza wafanyakazi mwanzoni mwa mwaka 2026, baada ya mahitaji ya bidhaa kupungua mara msimu wa sherehe za mwisho wa mwaka utakapopita, utafiti mpya umebaini.

Utafiti wa Maafisa Wakuu Watendaji uliofanywa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) unaonyesha kuwa uagizaji wa bidhaa, kiwango cha uzalishaji na idadi ya wafanyakazi vinatarajiwa kupungua katika robo ya kwanza ya 2026 ikilinganishwa na robo ya mwisho ya mwaka huu.

Kupungua huku kunatarajiwa kufuatia ongezeko la shughuli za kibiashara kutokana na msimu wa sherehe katika robo ya mwisho ya 2025, hali inayolingana na takwimu za hivi karibuni zilizoonyesha kuimarika kwa uzalishaji na ajira kutokana na matumizi makubwa ya mwisho wa mwaka.

Utafiti wa CBK kuhusu Maafisa Wakuu Watendaji wa makampuni huangazia matarajio ya baadaye, na unaonyesha tahadhari inayoongezeka miongoni mwa kampuni kuhusu uwezo wa kudumisha mahitaji baada ya matumizi ya msimu kupungua.

Maafisa waliohojiwa walisema mwelekeo huo ni wa kawaida baada ya sherehe, kwani familia nyingi hukaza matumizi mwanzoni mwa mwaka baada ya kutumia fedha nyingi Desemba.

“Uagizaji wa bidhaa, kiwango cha uzalishaji na idadi ya wafanyakazi vinatarajiwa kupungua, kuashiria kudorora kwa shughuli za kibiashara katika robo ya kwanza huku athari za msimu wa sherehe zikififia,” CBK ilisema.

“Hata hivyo, bei za mauzo na ununuzi zinatarajiwa kubaki thabiti kwa kiasi kikubwa, ingawa zitapanda kidogo,” utafiti ulisema.

Utafiti huo uliwalenga wakuu wa zaidi ya kampuni 1,000 kutoka sekta mbalimbali zikiwemo fedha, viwanda, ukarimu, mali isiyohamishika, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), kilimo na huduma za kitaaluma.