Wafanyakazi watatu wa kampuni ya ndege wakana kuiba sh13.7 M
WAFANYAKAZI watatu wa kampuni ndege wameshtakiwa kwa wizi wa Sh13.7m katika muda wa miezi 23.
Mabw Joshua Kipruto Ng’etich, Ernest Njenga Thiiru na Derrick Kiprono Ng’eno wa African Airline Association (AAA) waliokabiliwa na mashtaka sita ya wizi na ughushi wa stakabadhi walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Desemba 19,2025.
Watatu hap walikana mashtaka sita yaliyowasilishwa dhidi yao na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Renson Ingonga.
Mahakama iliambiwa washtakiwa walitekeleza wizi huo kati ya Januari 1,2022 na Novemba 21,2023.
Shtaka la pamoja dhidi yao lilisema kwamba walikula njama za kuibia AAA Sh13,756,798.
Ng’etich ambaye alikuwa mhasibu alikabiliwa na mashtaka mawili ya wizi na ughushi wa wasifu wa makubaliano wa kampuni ijulikanayo kwa jina Blue North Solutions Limited
Alidaiwa aliiba Sh13,756,798 kati ya Januari 1,2022 na Novemba 21,2023 mali ya AAA.
Mhasibu huyu alidaiwa aliiba pesa hizo alipokuwa akihudumu katika afisi za AAA zilizoko eneo la South C jijini Nairobi kaunti ya Nairobi.
Ng’etich na Thiiru wameshtakiwa kwa pamoja kuiba kitita hicho cha pesa walizozifikia kutokana na nyadhifa zao katika AAA.
Ng’etich alikuwa mhasibu naye Thiiru alikuwa agenti wa benki wa kampuni hiyo ya ndege inayohudumu kutoka uwanja wa ndege wa Wilson Airport.
Ng’etich pamoja na kampuni ya Blue North Solutions Limited walishtakiwa kuibia AAA Sh4,220,069.
Pia Ng’etich alikana alighushi stakabadhi za kampuni ya Blue North Solutions Limited akidai zilikuwa halali kwa vile zilikuwa zimetiwa sahihi na Symon Peter Cheruiyot.
Ng’eno na kampuni ijulikanayo Newmark Business Solutions walishtakiwa kuibia AAA Sh4,580,340.
Washtakiwa hao waliomba korti iwaachilie kwa dhamana huku wakiahidi hawatatoroka ila watafika mahakamani kila wakati watakapohitajika.
Upande wa mashtaka haukupinga watatu hao wakiachiliwa kwa dhamana.
Katika uamuzi wake hakimu aliamuru Ng’etich na Thiiru walipe dhamana ya Sh2milioni naye Ng’eno aliyekabiliwa na shtaka moja la kuibu Dola za Kimarekani $35,520 alipe dhamana ya Sh1milioni.
Endapo Ng’etich na Thiiru watashindwa kupata dhamana ya Sh2milioni, kila mmoja aliagizwa alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh600,000.
Naye Ng’eno alipewa dhamana badala ya Sh300,000.
Kesi hiyo itatajwa Januari 6,2026 kutengewa siku ya kusikizwa.
Wafanyakazi hao hawakulipa dhamana hiyo na walipelekwa gereza la viwandani wakisaka pesa za kujinusuru.
Hakimu aliamuru upande wa mashtaka uwape washtakiwa hao nakala za mashahidi waanze kuandaa tetezi zao.