Habari

Kenya One waapa kupangua hesabu ya Rais Ruto 2027

Na Collins Omulo December 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MUUNGANO mpya unaendelea kuibuka katika ulingo wa siasa za kitaifa nchini Kenya, ukijisawiri kama sauti mbadala dhidi ya miungano mikuu huku ukiweka wazi azma yake kuu ni kumfanya Rais William Ruto kuwa rais wa muhula mmoja pekee katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Muungano huo hauegemei Kenya Kwanza, serikali jumuishi wala Muungano wa Upinzani.

Badala yake, unawaleta pamoja wabunge vijana kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa wanaotaka kujinasua kutoka kivuli cha vyama vyao na kujijenga kama mrengo mpya wa kisiasa.

Muungano huu unalenga kuvunja utamaduni wa muda mrefu wa siasa za “farasi wawili” na kujitangaza kama chaguo mbadala kwa wapiga kura waliokata tamaa.

Chanzo cha Kenya Moja kinahusishwa na maandamano ya kizazi cha Gen Z ya mwaka 2024, pamoja na kuundwa kwa serikali jumuishi kati ya Rais Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, aliyefariki Oktoba 15.

Viongozi wa Kenya Moja wanasema makubaliano hayo yaliwasaliti wananchi na kuzima sauti ya upinzani bungeni.

Wanasema ni muhimu kuwa na muundo mpya wa kisiasa unaowakilisha vijana na kupinga siasa za ukabila ambazo nchi imezoea.

Muungano huo unaongozwa na Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.

Wengine ni pamoja na Gathoni Wamuchomba (Githunguri), Jack Wamboka (Bumula), Anthony Kibagendi (Kitutu Chache), Clive Gisairo (Kitutu Masaba), Obadiah Barongo (Bomachoge Borabu), Joshua Kimilu (Kaiti) na Majimbo Kalasinga (Kabuchai).

Viongozi hao wamekuwa wakipinga vikali serikali jumuishi, wakisema imesababisha bunge kuwa kibaraka wa utawala wa serikali na kupoteza uhuru wa kuangazia masuala yanayohusu wananchi.

Babu Owino amekuwa akivutana na ODM kutokana na azma yake ya kuwania ugavana wa Nairobi, akisisitiza kwamba huenda asipate haki ndani ya chama kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya serikali jumuishi.

Seneta Sifuna naye amesisitiza hatambui serikali kwa jina hilo, na hata kutishia kujiuzulu kama katibu, iwapo ODM itaamua kumuunga mkono Rais Ruto 2027.

Kenya Moja inalenga kuvutia kura za vijana, wanaokadiriwa kufikia milioni 14 kufikia uchaguzi ujao. Viongozi wake wanajitambulisha kama kizazi kipya kinachopigania uwazi, mageuzi ya kiuchumi na siasa zisizoegemea ukabila.

“Haya ni mapambano ya kizazi, kati ya wanaolinda mfumo wa zamani na viongozi vijana,” alisema Amisi.

Wanaeleza wazi kuwa wanataka kubadilisha mfumo wa kisiasa na kutoa nafasi kwa vijana kuingia madarakani.

Kwa mujibu wao, kundi hilo si mrengo wa tatu pekee kuelekea uchaguzi mkuu ujao, bali linajitambulisha kama sauti ya kweli ya wananchi ambao wamekata tamaa na vyama vikuu vya kisiasa.

Wanasema lengo lao kuu ni kuunda mfumo unaowajibika, kuangalia masuala ya uchumi, na kuhakikisha heshima kwa katiba na haki za raia.

“Si mapambano ya ubinafsi, bali ni mapambano ya kitaifa,” alisema Sifuna.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanashuku uwezo wa Kenya Moja kudumu katika ulingo wa siasa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kimaifa cha Amerika, Profesa Macharia Munene anasema muungano huo ni sehemu ya mbwembwe za kisiasa zinazoibuka kadri uchaguzi unavyokaribia.

“Kenya Moja inalenga kuzua kelele tu ili waweze kutambuliwa na wagombeaji wakuu. Uchaguzi wa 2027 bado utabaki kuwa kati ya wagombea wawili wakuu,” alisema.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua naye amepuuza muungano huo, akisema Wakenya hawako tayari kwa mrengo wa tatu.

Wachambuzi wa siasa Joshua Nyamori na Javas Bigambo wanasema Kenya Moja haina mizizi ya kiitikadi wala muundo wa chama, na hivyo hauwezi kuwa nguvu halisi ya kisiasa.

Wanasema muungano huu ni sawa na jaribio la kutaka kuonekana tu na kutafuta nafasi ya kuzungumza na vyama vikuu.

Hata hivyo, licha ya ukosoaji huo, Kenya Moja inaendelea kujitangaza kama sauti ya kizazi kipya.

Viongozi wake wanasema hawataogopa changamoto yoyote na wataendeleza juhudi za kupigania maslahi ya wananchi. Wanasisitiza kuwa mradi wao ni wa muda mrefu na unalenga kudumu hadi uchaguzi ujao.