Habari za Kitaifa

Serikali yapiga darubini madaktari watoro wanaoshinda katika kliniki za kibinafsi

Na ERIC MATARA December 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI itawachukulia hatua madaktari wanaolipwa kwa pesa za umma huku wakiacha majukumu yao katika hospitali za serikali na kuendesha kliniki zao binafsi.

Wizara ya Afya inasema tabia ya madaktari kuhepa kazi mara kwa mara, hasa katika hospitali za kaunti na zile za rufaa, imesababisha wagonjwa wanaohitaji upasuaji na huduma muhimu kuhangaika.

Katika baadhi ya visa, wagonjwa hupewa tarehe za matibabu zilizo mbali katika hospitali za umma, kisha kufuatwa na mapendekezo ya kwenda hospitali za kibinafsi ambako madaktari hao hao wanahudumu.

Akizungumza Jumatano, Waziri wa Afya Aden Duale alisema serikali imechoshwa na mwenendo huo na itaanza msako mkali kuanzia Januari.

Alisema madaktari wanaofanya kazi kwingine ndani ya saa rasmi za kazi wanajihusisha na ulaghai na watachukuliwa hatua kali.

Aliongeza kuwa Mamlaka ya Afya ya Kidijitali imeagizwa kuchukua hatua dhidi ya madaktari wanaowasilisha malipo ya bima katika hospitali za kibinafsi ilhali wameajiriwa kufanya kazi katika hospitalini za umma.

Magavana kadhaa wameunga mkono hatua hiyo wakisema tatizo hilo ni kubwa na linaathiri juhudi za kufanikisha mpango wa afya kwa wote.

Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, alisema madaktari lazima wabaki hospitalini kuwahudumia wananchi badala ya kugeuza hospitali za umma kuwa maeneo ya kupata wateja wa kliniki za kibinafsi.

Naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Muthomi Njuki, alisema madaktari wengine hutumia sehemu ndogo tu ya muda wao hospitalini kisha wanaenda kliniki za kibinafsi licha ya kupokea marupurupu maalum yanayolenga kuwazuia kufanya kazi za kibinafsi.

Alionya kuwa kaunti hazitasita kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, Njuki alisimulia jinsi alivyofanya ziara ya ghafla katika hospitali na kukuta madaktari kadhaa hawakuwa kazini na baadaye akabaini walikuwa wakihudumia wagonjwa katika kliniki zao binafsi.

Alisema baadhi ya wagonjwa hulazimika kulipia matibabu mara mbili.