Habari za Kitaifa

Mikakati mipya ya serikali yazima ujangili Bonde la Ufa

December 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA kipindi cha miezi sita sasa, utulivu umeanza kurejea taratibu katika Bonde la Kerio lililojishindia jina la ‘Bonde la Mauti’ kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara.

Mashambulizi hayo ambayo yameendelea tangu mwanzoni mwa mwaka huu yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 22 katika kaunti za Baringo na Elgeyo Marakwet.

Hata hivyo, wakazi wameanza kurejelea shughuli zao za kawaida kutokana na operesheni ya usalama iliyoanzishwa na serikali ili kurejesha utulivu.

Kwa miaka mingi, serikali ilikuwa ikitumia operesheni kali ya kutwaa silaha katika maeneo yanayosheheni majangili Bonde la Ufa Kaskazini.

Lakini licha ya kutuma vikosi mbalimbali kuwapokonya raia silaha, ilikuwa nadra kwa juhudi hizo za kuondoa bunduki kuzaa matunda kwa sababu mashambulizi zaidi yaliripotiwa na wanajamii kuendelea kusafirisha silaha kimagendo.

Wataalamu wa usalama walikuwa vilevile wameonya kwamba serikali haingefanikisha azma yake ya kutwaa bunduki pasipo kuainisha maeneo lengwa, wakipendekeza kubadilisha mikakati na mipango kabambe katika vijiji vilivyoathirika.

Mwaka huu, serikali iligeukia kubadilisha mikakati ili kurejesha hali ya kawaida katika vijiji vilivyogubikwa na ukosefu wa usalama na kuchagua oparesheni inayoongozwa na ujasusi kuwalenga washukiwa wa uhalifu badala ya wanajamii wote.

Akizuru miji ya Marigat na Kabarnet, Kaunti ya Baringo, mwezi mmoja uliopita, Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, aliashiria kwamba kupitia mikakati iliyowekwa na serikali, utulivu umerejeshwa katika Bonde la Kerio.

Kulingana na waziri huyo, zaidi ya bunduki haramu 600 zimesalimishwa kwa hiari na wakazi eneo hilo, 300 miongoni mwake zikitoka Baringo.

“Baadhi ya kaunti katika Bonde la Ufa Kaskazini zilivurugika kabisa kutokana na itkadi za kijadi za wizi wa mifugo na ujangili, lakini kwa sababu ya juhudi za serikali, hali ya kawaida imerejeshwa katika vijiji vilivyoathirika,” alisema Waziri Murkomen wakati huo.

“Tutahakikisha bunduki zote zilizo mikononi mwa raia zimetwaliwa ili wakazi waishi kwa amani. Hatutaafikiana na viongozi wa kisiasa wanaotatiza mchakato huo. Hakutakuwa na kushirikisha umma kuhusu masuala ya kutwaa bunduki au majadiliano yoyote. Operesheni itaongozwa na ujasusi,” alisema Waziri.

Kamanda wa Polisi Elgeyo Marakwet Peter Mulinge, alisema walianzisha oparesheni ya ujasusi inayolenga washukiwa wa uhalifu, waliohitajika kusalimisha silaha haramu wanazomiliki.

“Operesheni hiyo ilifanikiwa kwa sababu tulichukua muda kuanisha maeneo yaliyoathirika na kuwatambua washukiwa wa uhalifu waliojihami badala ya kulenga jamii yote.

“Tulifaulu kuwakamata kadhaa, waliosalimisha kwa hiari bunduki haramu walizokwamilia, na serikali kuu na ya kaunti iliwasaidia kupata namna mbadala ya kujikimu kimaisha,” alisema Bw Mulinge.

Kikosi jumuishi kinachoendesha oparesheni ya usalama katika maeneo yanayohangaishwa na majangili, kikisaidiwa na polisi wa akiba nchini, kiliweza kuwatimua wahalifu waliojihami na kuimarisha maeneo – hatua iliyorejesha utulivu na kuhimiza wakazi waliofurushwa kurejea makwao.

Machi mwaka jana, kwa mfano, kikosi jumuishi kinachoendesha operesheni Baringo kililipua kwa bomu Bonde la Tandare, moja kati ya maeneo yaliyoorodheshwa kama maficho ya majangili Baringo Kusini.

Kulingana na Kamanda wa Polisi Baringo, Julius Kiragu, wakisaidiwa na kikosi hicho, walitekeleza vilevile uangalizi angani uliosaidia kufuatilia maficho ya washambulizi waliojihami.

Kanali (Rtd) Moses Kwonyike, aliyehudumu kama mshauri wa kijeshi na mkuu wa Operesheni ya Afrika ya Umoja wa Mataifa Darfur, alisema serikali ilipasi safari hii kwa kubadilisha mikakati ya kujenga amani Bonde la Ufa Kaskazini lililosambaratishwa na mapigano.

Safari hii, serikali hata ilifahamu ni nani aliyeiba mifugo siku iliyotangulia, na waliiendea,” alisema mwanajeshi wa zamani ambaye kwa muda mrefu amepinga upokonyaji silaha kimabavu.

“Wahalifu walikuwa wanatudhihaki waliposikia kuhusu oparesheni mpya ya kutwaa silaha, wangetorokea vijiji vilivyo mashinani ambapo hawangepatikana, na kuwaacha raia wasio na hatia – ikiwemo wanawake na watoto – kuteseka mikononi mwa maafisa wa usalama.

“Safari hii, majangili walifurushwa kutoka mafichoni mwao na wakashurutishwa kusalimisha bunduki haramu,” alisema Richard Chepchomei, mkazi katika kijiji kinachogubikwa na ukosefu wa usalama, Chemoe, Baringo Kaskazini.

Alisema mwelekeo wa serikali unaolenga wahalifu na kutwaa silaha ndio bora, kinyume na kulenga jamii zima jinsi ilivyokuwa mbeleni.