Habari za Kitaifa

‘Homa’ kali ya Krismasi yavamia Wakenya tena

Na WAANDISHI WETU December 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWAKA unapoelekea kuisha, msisimko wa sherehe unaendelea kutanda kote nchini wengi wakilazimika kujimudu licha ya uchumi mgumu, hali ya anga isiyotabirika pamoja na ubabe wa kisiasa.

Maelfu ya Wakenya wamechagua kudumisha desturi ya kujiunga na jamaa zao vijijini kwa sikukuu kama miaka ya nyuma japo mara hii hali ngumu ya maisha inaonekana kuwalemea wengi.

Magharibi, eneo ambalo yamkini ndilo linalokumbatia sana sikukuu ya Krisimasi kwa Wakenya, aghalabu hushuhudia ongezeko la wasafiri wenye hamu ya kuungana na familia zao.

Kamishina wa Eneo la Nyanza Flora Mworoa, alisema vikosi vya usalama vimeshirikiana na Shirika la Wanyamapori (KWS) kuimarisha usalama katika sekta ya utalii.

Vikosi vya usalama vilevile vinashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) kuhakikisha madereva wanazingatia sheria za trafiki ili kuzuia ajali.

Kulingana na ripoti iliyotolewa majuzi na Huduma ya Polisi nchini, sehemu hatari Magharibi mwa Kenya zinajumuisha barabara za Mbale–Vihiga, Kakamega–Chavakali, Kakamega–Kisumu–Ilesi, Museno, Kakamega–Mumias Road, Makunga, na barabara kuu ya Kakamega–Webuye–Lubao.

Eneo la Nyanza itabidi usalama umakinikiwe zaidi barabara za Awasi–Ahero Kiboswa–Kisumu, Oyugis–Kisumu, Migori–Kakrao, Makutano ya Daraja Mbili–Bondo na barabara ya Oyugis–Katitu.

Jiji la Kisumu limeweka kando usingizi na kugeuka sherehe waziwazi ambapo muziki unafuatana na baruti hewani huku kila jioni ikiahidi kumbukumbu mpya za ngoma ambazo wakazi wanaita “sherehe baada ya sherehe (party after party).”

Katika eneo la Pwani, wamiliki hoteli walikiri kupokea zaidi ya asilimia 80 ya wageni katika majengo yao, wakitumai kwamba idadi hiyo itafikia asilimia 90–100 kufikia Krismasi na Mwaka Mpya.

Msimamizi wa Hoteli ya Malindi Ocean Beach Resort and Spa, Maureen Obunga, alisema karibu nusu ya wageni inajumuisha Wakenya kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Mkuu wa Majeshi, Charles Kahariri alizuru Msitu wa Boni, Lamu, kushiriki tamasha za mapema za Krismasi na Mwaka mpya huku wanajeshi wakitumwa kukabiliana na magaidi wa Al-Shabaab.

Doria za kiusalama zimezidishwa Bonde la Ufa huku Kamanda wa eneo hilo, Dkt Abdi Hassan, akiwahimiza waendeshaji magari kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Hoteli kubwa kadhaa Naivasha na Nakuru zimeandikisha idadi kubwa ya wageni kabla ya Krismasi zikiripoti takriban asilimia 96, Naivasha, na kati ya asilimia 80-90, Nakuru.

“Tunatarajia biashara bora zaidi ikilinganishwa na mwaka jana, na hicho ni kitu tunajivunia,” alisema Mwenyekiti wa Muungano wa Utalii Nakuru, David Mwangi.