Waiguru: Ruto bado ndiye baba lao Mlima Kenya
GAVANA wa Kirinyaga amekashifu upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akisema kushambulia serikali bila kutoa suluhu ni kazi bure.
Bi Waiguru alisema kuwachochea raia dhidi ya serikali hakutasababisha upinzani upate uungwaji mkono hasa ukanda wa Mlima Kenya.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bi Waiguru alisema upinzani unajidaganya kwa kufikiria kwamba kuangazia changamoto za utawala wa Rais William Ruto kutasababisha wapate uungwaji mkono.
“Ni jambo moja kumkashifu Rais Ruto lakini wakazi wa Mlima Kenya wanastahili kufikiria kile ambacho serikali itawatimizia. Upinzani unamakinikia tu kugawana mamlaka,” akasema Bi Waiguru.
Bi Waiguru pia alionya kuhusu juhudi zozote za kusawiri Mlima Kenya kama eneo ambalo linatumia idadi yake kudharau maeneo mengine kuhusu kura wanazopiga kwenye uchaguzi mkuu.
Kauli yake ilikuja wakati ambapo ubabe wa kisiasa unaendelea nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Upinzani ukiongozwa na Bw Gachagua hasa unalenga kuhakikisha kwamba unajizolea uungwaji mkono Mlima Kenya ambako rais alipata kura nyingi 2022.
Gavana huyo alisema Kenya Kwanza imedhibiti uchumi, kulipa madeni na kila mahali nchini kuna mradi ambao umeanzishwa na serikali.
Alikiri kwamba umaarufu wa Rais Ruto umepungua sana eneo la Mlima Kenya ikilinganishwa na 2022 ila akasema kuna watu wengi ambao wanaunga mkono utawala wa sasa kimya kimya.
“Upinzani unaonekana umeamini kuwa kwa kutambua udhaifu wa serika ya Kenya Kwanza watashinda uchaguzi. Hata hivyo, wapigakura sasa ni werevu na watatumia miradi iliyoanzishwa kuiunga serikali au kuiangusha,” akasema Bi Waiguru.
Huku madai yakizuka kuwa baada ya kukamilisha muhula wake 2027 atauwania Useneta, Bi Waiguru alisema bado mashauriano yanaendelea na yupo tayari kudumu kwenye wadhifa wowote ule.
Bi Waiguru ametumikia serikali katika nyadhifa mbalimbali na alikuwa waziri wa ugatuzi ambapo alianzisha Huduma Centers ili kuleta huduma karibu na wananchi.
Pia alichaguliwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (COG) wadhifa ambao aliushikilia kwa muda wa miaka miwili.
“Majukumu hayo yalinoa uweledi wangu katika masuala ya uongozi ndiyo maana nipo tayari kuwahudumia Wakenya kwenye ngazi nyingine za utawala,” akasema.
“Nalenga kusalia kwenye siasa na masuala ya uongozi ndiposa baada ya 2027 nipo tayari kuwatumikia Wakenya kwenye wadhifa mwingine,” akasema.
Kuhusu rekodi yake ya maendeleo kama gavana wa Kirinyaga, Bi Waiguru alijinaki kuwa amepandisha hadhi Hospitali ya Kaunti na Rufaa ya Kerugoya kutoka Level 4 hadi 5.
Pia alitaja kukarabatiwa na kupandishwa hadhi kwa Hospitali za Kimbimbi, Kianyaga na Sagana kutoka Level 3 hadi 4.
Aliongeza kuwa amehakikisha kuna dawa na huduma bora katika vituo 24 vya afya.
Katika sekta ya kilimo zaidi ya nyumba 100,000 sasa zinajitosheleza kichakula baada ya kupigwa jeki na kaunti kupitia mpango wa Wezesha Kirinyaga.
Vilevile alijinaki kuwa wakazi wengi sasa wanaweza kuyapata maji kwa urahisi kinyume na hapo awali.