Vicheche wa usiku walia Gen-Z kuingilia biashara yao
ELDORET MJINI
WACHUUZI wa miili katika kituo cha baishara cha Juakali jijini Eldoret wameelezea kusikitishwa kwao na idadi kubwa ya wanafunzi waliojitosa katika biashara hiyo na kuchukua wateja wao ambao huvutiwa na damu changa.
Mmoja wa wahudumu hao ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema awali biashara hiyo ilikuwa nzuri lakini siku hizi imeharibika hasa baada ya chipukizi wa Gen-Z kujitosa ndani.
“Kitambo biashara ilikuwa nzuri ambapo tulikuwa na wateja wengi lakini siku hizi hawa watoto mnaita Gen-Z wametuharibia biashara kwa kujitoza katika biashara yetu haswa msimu huu wa likizo,” alisema mmoja wa wahudumu hao.
Mama huyo alifichua kuwa baadhi ya chipukizi hao ni wanafunzi wa shule za msingi na upili ambao hufika katika kituo hicho usiku kuburudisha waendeshaji malori ya masafa marefu ambao hukesha katika kituo hicho kwenye barabara kuu ya Eldoret-Uganda.
Kutokana na changamoto hiyo, wakongwe wameapa kuanza kufurusha wasichana wadogo katika maeneo yao ya kazi.
“Hatungependa kuacha watoto waendelee kuharibika, hata sisi ni wazazi na hii si biashara ya kuruhusu watoto wafanye, ni hali ngumu inatutuma katika biashara hii,” aliongeza.