Sikukuu ya kilio na majonzi kwa wahanga wa machafuko Narok, Kapedo
ZIKIWA zimesalia saa zaa kuhesabika tu kabla ya sikukuu ya Krismasi kuwadia, kwa baadhi ya Wakenya hakuna cha kusherehekea kutokana na masaibu chungu nzima yanayoendelea kuwaandama.
Mbali na uchumi mgumu ambao umewasakama wengi, Wakenya ambao wanaishi katika maeneo ya Narok, Kapedo na walioathiriwa na ajali nyingi za barabarani wakisafiri kuenda kujiunga na jamaa zao, hawana chochote cha kusherehekea.
Kwa wakazi wa Kapedo, hakuna chochote cha kusherehekea wala hakuna hata chakula au shamrashamra zinazoendelea kama kuwanunulia watoto nguo mpya.
Hii ni kwa sababu wajane wengi bado wana makovu ya mauaji na madhila waliyoyapitia mikononi mwa majangili.
Kapedo inapatikana katika mpaka wa Kaunti za Turkana na Baringo ambako wizi wa mifugo umekuwa ukishuhudiwa na mauaji yasiyomithilika kutokea.
Ikilinganishwa na miaka ya awali, angalau kuna utulivu kidogo hasa katika Bonde la Suguta ambalo linafahamika kwa mauaji.
Kwa mjane Limangole Ekiru, mama wa watoto wanane, hana cha kusherehekea baada ya familia yake kusambaratishwa na ujangili.
Bi Ekiru anasema kuwa kwake la muhimu ni kuendelea kuishi tu akipambana na makali ya njaa.
Bi Ekiru, 65, amebeba maji ya lita tatu mgongoni mwake na mfuko wenye matunda ya mwituni.
Amesafiri kilomita 10 chini ya jua kali akiwa pia amebeba vifaa kutoka kichakani vya kutengeza fagio kisha kuziuza ili aendelee kujikimu.
Simulizi kutoka kwake inasema mumewe Francis Ekiru aliuawa na majangili mnamo 2009 akiwachunga mbuzi wao.
Majangili hao waliiba zaidi ya mifugo 30 waliokuwa kitega uchumi chao. Bila mume na mifugo, alianza kuuza kuni katika kituo cha kibiashara cha Kapedo.
Hata hivyo, aliasi biashara hiyo kutokana na kuongezeka kwa visa vya ujangili kwa sasa yeye na jamaa wengine wa familia wakitegemea chakula cha msaada kinachotolewa na serikali.
“Walichukua kila kitu, sina mume na watoto wangu watatu baadaye waliaga dunia kutokana na magonjwa yanayosababishwa na makali ya njaa. Wengine watatu waliacha shule kutokana na ukosefu wa karo na wengine ni wadogo,” akasema.
Hali ni hiyo kwa Lilian Ejore, 38, ambaye mumewe Henry Ejore alikuwa chifu kabla ya kuuawa mnamo 2017.
Alipatwa na mauti akiwatetea wanakijiji dhidi ya uvamizi wa majangili eneo jirani la Lomelo.
Kutokana na uvamizi huo, Bi Lilian alitoroka na watoto wao wanne wala hana namna kwa sababu alikuwa akimtegemea sana mumewe kuwakimu.
“Sasa ninatengeneza vifagio kuwakimu watoto wangu na nategemea basari kuwasomesha pamoja na Sh2,000 kila mwezi zinazotolewa kwa wajane na serikali. Hii Krismasi itapita tu kwa sababu sina pesa au namna, kila ufagio nauza kwa Sh15,” akasema Bi Lilian.
Kwingineko, katika eneo la Trans Mara, Kaunti ya Narok hakuna chochote cha kujivunia Krismasi hii baada ya serikali kutangaza kafyu kutokana na vita kati ya jamii tatu za mahali hapo.
Watu wanne wameaga dunia na zaidi ya 1,800 kulazimika kuhama makwao huku polisi nao wakiweka marufuku ya kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi.
Jamii tatu zimekuwa zikizozana vikali katika wadi za Ang’ata Barikkoi, Lolgorian na Keyian.
Maeneo ambako kutakuwa na Krismasi ya kafyu ni Nkararu ya Trans Mara Magharibi, na Oldonyo-Orok, Siteti, Ololoma, Corner, Ratiki, Isokon, Kerinkani, Kondamet, Olkiloriti, Angata Barakoi, Kapkures, Lolgorian town, Mashangwa na Sachangwan, Trans Mara Kusini.
Mbali na hayo, kumekuwa na misururu ya ajali za barabarani, tukio la hivi punde likiwa kuteketezwa kwa basi la Mash Poa katika eneo la Salgaa, Nakuru.
Basi hilo lililokuwa limewabeba abiria 60 lilichomwa na wahudumu wa bodaboda wenye hasira baada ya mmoja wao kugongwa na kufariki papo hapo.
“Baadhi ya abiria walilazimika kuhepa kwa kuruka kupitia madirishani. Dereva alijibizana na wahudumu hao kabla ya basi kuteketezwa naye akatorokea usalama wake,” akasema James Mwangi aliyeshuhudia tukio hilo.