Namna mwili wa Raila ulivyofika bungeni usiku
DAKIKA chache kabla ya usiku wa manane mnamo Oktoba 16, 2025, mkutano uliochukua muda mrefu kupanga jinsi ya kuulaza mwili wa aliyekuwa waziri mkuu, Raila Odinga bungeni, ulikamilika katika jengo la bunge.
Kikao hicho kilikuwa cha siri mno hivi kwamba hata wabunge wengi hawakufahamu kukihusu na wafanyakazi walioshirikishwa katika maandalizi walionywa kuhusu adhabu kali endapo habari zingevuja kwa vyombo vya habari.
Mkutano huo ulioanza saa nne usiku, ulikamilika usiku wa manane na mwili wa Odinga kuwasili bungeni saa kumi na moja alfajiri, Oktoba 17, kabla ya kuelekea katika Uwanja wa Michezo wa Nyayo kwa ibada ya mazishi ya kitaifa.
Duru zilizohudhuria kikao hicho zilidokezea Taifa Leo kwamba walitoka bungeni usiku wa manane na kurejea saa tisa usiku wa manane, tayari kuhakikisha mchakato huo unaendelea ulivyopangwa.
“Hata sikumwambia mke wangu nilipokwenda saa tisa usiku wa manane kwa sababu hapo haungemwamini mtu yeyote na habari kama hizo,” afisa huyo alieleza.
Ripoti za awali za ujasusi zilizosambazwa na uongozi wa bunge ziliashiria kuwa halaiki ya watu waliokuwa na hamu ya kuutazama mwili wa aliyekuwa kinara wa ODM huenda ingehatarisha usalama bungeni.
“Kulikuwa na hofu kwamba tungeshuhudia uvamizi mwingine wa bunge sawa na ilivyofanyika wakati wa maandamano ya Gen-Z, hivyo basi tulilazimika kuwaza kuhusu njia nyingine ya kuhakikisha mwili wa Raila unaletwa kwa sababu hatua hiyo ilikuwa muhimu kwa historia yetu na kuheshimu huduma zake kwa nchi, afisa mwingine akaeleza.
Uongozi wa Bunge, hata hivyo, haukuwa tayari kufa moyo kuhakikisha kwamba Bw Odinga aliyehudumu bungeni kama mbunge wa eneobunge la Lang’ata hangekuwa sehemu ya historia na rekodi za bunge kwa kukosa kulazwa katika taasisi hiyo.
“Hakuna vile tungeruhusu baadhi ya watu wahuni kutuzuia kuleta mwili wa Raila bungeni,” akasema mbunge aliyekuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano wa usiku.
Kikao hicho kilihudhuriwa vilevile na wasaidizi wa bunge na wawakilishi kutoka Huduma ya Polisi hasa waliomo Nairobi kwa mpangilio madhubuti.
Waandalizi walikuwa na uhakika kwamba sehemu kubwa ya umma ingewasili Uwanja wa Nyayo alfajiri ambapo ibada ya mazishi ya kitaifa ingefanyika na wala sio katikati ya jiji kuu ambapo wangegundua maandalizi yasiyo ya kawaida kiusalama bungeni na kuingia.
Waandalizi waliafikiana kwamba ni wabunge wachache tu wangearifiwa ili kuzuia habari kusambazwa kwa umma ambao ungejitokeza Ijumaa, hali ambayo huenda ingevuruga mchakato huo tena.
Wabunge wachache wapatao 36 kutoka Bunge la Kitaifa na maseneta 12 waliarifiwa kuhusu uamuzi huo na kuagizwa kufika asubuhi saa moja kamili kutazama mwili.
Saa tisa usiku wa manane, wabunge wengine 10 na maseneta watano waliarifiwa kwamba mwili wa Odinga utakuwa katika majengo ya bunge hivyo basi wajitokeze kuutazama na kuepuka kupanga foleni uwanjani Nyayo pamoja na watu wengine wakati wa ibada ya kitaifa.
“Tulijiepusha na wabunge ambao wangechapisha habari hizo kwenye mitandao ya kijamii na kuvutia watu bungeni, tulichagua wale wenye urazini pekee,” zikasema duru.
Wabunge wengine walifahamishwa asubuhi saa moja wakati polisi walikuwa wameimarisha doria huku mwili wa Odinga ukielekea kuwasilishwa bungeni.
Mchakato wote uliendelea vyema ambapo wabunge wapatao 163 wakiongozwa na Rais William Ruto pamoja na familia ya Odinga walitoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Odinga uliopelekwa baadaye Nyayo Stadium kwa ibada ya kitaifa.
Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge alikiri mpango huo uliwekwa siri kwa maslahi ya umma na bunge.
Alisema hakukuwa na nia mbaya kutenga umma kwa sababu hafla iliyofanyika bungeni ilikuwa fupi na ya kihistoria kutokana na hadhi ya Bw Odinga aliyehudumu kama waziri mkuu.