Makala

Hofu familia ikiagiza wakazi walihame shamba la Sh3.9b

Na BRIAN OCHARO December 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI na wawekezaji katika sehemu za Kisiwa cha Wasini wanaishi kwa hofu msimu huu wa sikukuu ya Krismasi, baada ya familia ya Saggaf, iliyopewa hatimiliki ya ardhi hivi majuzi, kutoa ilani ya kuwataka wahame.

Hatua hiyo imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wawekezaji, wamiliki wa hoteli na familia za wenyeji ambao wanategemea mapato ya kilele cha utalii mnamo Desemba.

Ilani hiyo, iliyotolewa kupitia mawakili wa familia, inawaelekeza wenyeji kuondoka ndani ya siku 90 na kuondoa miundo yote iliyojengwa kwenye kipande cha ardhi chenye thamani ya Sh3.9 bilioni. Iliendelea kusema kuwa, kutokufuata maagizo hayo kutasababisha hatua za kisheria.

Wasimamizi wa ardhi hiyo Mohamed Maula Saggaf na Ali Abad Abubakar Nassir Mkulu wameshutumu waekezaji na wakazi wa eneo hilo kwa kuingia kinyume cha sheria na kujenga miundo bila ridhaa au ruhusa.

“Kuendelea kukaa kwenye ardhi hiyo kunachukuliwa kama kuingilia kwa njia isiyo halali haki za miliki ya familia ya Saggaf,” ilani hiyo inasema.

Hata hivyo, wenyeji wamepewa fursa ya kujadili uwezekano wa kukodisha ardhi au kununua kupitia mawakili wa familia ndani ya kipindi kilichotolewa.

Eneo hilo linajumuisha miundo kadhaa ya huduma za utalii inayotegemea mapato ya msimu wa sikukuu, pamoja na familia ambazo zinasema kuwa zimeishi katika kisiwa hicho kwa miongo kadhaa. Kisiwa cha Wasini huvutia watalii wa ndani na kimataifa kwa shughuli za baharini.

Ilani hiyo ilitolewa miezi michache kufuatia kukamilika kwa mzozo wa muda mrefu wa ardhi ulioanza mwaka wa 1979, wakati kiongozi wa familia hiyo Abdulrahman Saggaf Alawy alipoanza kudai ardhi hiyo kutoka kwa wanyakuzi.

Familia hiyo ni miongoni mwa wakazi wa mapema wa Kisiwa cha Wasini, baada ya kuhamia eneo hilo kutoka Vumba Kuu karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania karibu miaka 400 iliyopita.

Mzozo huo umepitia kamati na tume kadhaa za serikali, ikiwa ni pamoja na Kamati ya Ukaguzi ya Saitoti, Uchunguzi wa Ardhi wa Njonjo, Tume ya Ardhi ya Ndung’u, Kamati ya Swazuri na Tume ya Gershon Otachi, iliyosababisha kutoa hati ya umiliki mwezi Septemba.

Wamiliki wa awali, Hassan, Mohamed na Ahmed Nassir, walihifadhi hati ya ardhi mwaka 1908, iliyoidhinishwa mwaka wa 1969 baada ya Kenya kupata uhuru.

Baadaye familia hiyo ilishinda kesi Mahakamani Mombasa mnamo 1995. Tume ya Taifa ya Ardhi ilitambua familia hiyo kama waathiriwa wa dhulma za kihistoria ambao ardhi yao ilinyakuliwa na kufutilia mbali hati zinazopingana kupitia taarifa rasmi mwaka wa 1997 na 2019.

Familia hiyo imeanza kudai ardhi yake kwa wawekezaji wa kibiashara, ikiwataka wazinunue kwa bei ya sasa au kuondoka. Vilevile, familia hiyo pia imeomba serikali kununua sehemu za ardhi ili kuwawezesha wapangaji wa muda mrefu kupata makazi yao.