Michezo

Kombe la Essie Akida kuanza rasmi Ijumaa Kilifi

Na TOTO AREGE December 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAKALA ya tatu ya Kombe la Esse Akida, yataanza rasmi Ijumaa Desemba 26, 2025 na  kukamilika Jumapili, Desemba 28, 2025, katika uwanja Mkoroshoni Community Grounds Kaunti ya Kilifi.

Akida ni mshambuliaji wa Harambee Starlets na pia mchezaji wa timu ya Kibera Soccer Women ya Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL). Alianzisha mashindano haya akilenga, kukuza talanta mashinani na kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kuonyesha talanta zao.

Mashindano hayo yamevutia timu 25 (20 za wanaume na tano za mabinti) kutoka wadi za Kaunti ya Kilifi kama; Mnarani, Kibarani, Sokoni na Kibaoni.

Timu ya Blue blue upande wa wanaume (mabingwa mara mbili) na Kilifi Elite Women wanapigania kutetea ubingwa wao katika makala ya mwaka huu. Timu tatu bora zitaenda nyumbani na pesa, vikombe na jezi.

Mchezaji huyo wa zamani wa Thika Queens pia ni mwandishi na amechapishwa kitabu kwa jina Chained.

Kitabu hicho kilizinduliwa Agosti 31 mwaka jana na kinasimulia taaluma yake ya soka, ustahimilivu, vizuizi vya kitamaduni alivyokutana navyo, na changamoto nyingi alizo kabiliana nazo.

Ameelizea matatizo alokumbana nayo nyuma miaka ile akichezea Starlets, ligi ya ndani na kucheza soka ya kulipwa ughaibuni na uamuzi wake wa kutetea wasichana wadogo ambao sauti zao mara nyingi, hazisikiki.

Akida alikuwa sehemu ya timu ya Starlets ambayo ilishiriki kwa mara ya kwanza katika Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mwaka 2016 nchini Cameroon.