Wasanii watakavyopiga sherehe ya Krismasi leo
KWA Wakenya wengi, Krismasi ni zaidi ya siku ya kawaida kwenye kalenda, ni msimu wenye maana kubwa.
Ni wakati wa kusita, kurejea nyumbani na kujumuika na chimbuko lao na kukumbuka asili yao.
Kwa watu mashuhuri, msimu wa sherehe aghalabu una maana mbalimbali inayojumuisha familia, kumbukumbu, shukrani na nia, kila mmoja anaisherehekea kwa namna ya kibinafsi.
Taifa Leo Dijitali ilizungumza na wasanii kadhaa waliosimulia jinsi watakavyosherehekea Krismasi mwaka huu.
Mwimbaji Bien aliwahimiza mashambiki wake kuzipa familia zao umuhimu katika msimu huu wa sherehe, akiashiria shukrani na faraja kwa wanaokabiliwa na nyakati ngumu.
Alipoulizwa kuhusu kumbukumbu yake ya utotoni kuhusu Krismasi, Bien alisimulia itikadi za kanisa zilizoacha taathira ya kudumu.
“Ninakumbuka nikiimba Malako, wimbo wa Krismasi ambao aghalabu ulitumika kwenye mashindano ya kanisa. Tukiwa watoto, tulikuwa tunaimba na hata tukashinda tuzo,” alisema akitabasamu.
Mbunaji matini Milly Chebby anasema mwaka huu atasherehekea Krismasi nyumbani kwake Kiambu pamoja na marafiki wa karibu.
Mwanahabari Willy M Tuva naye atatumia muda mwingi wa Krismasi kazini lakini si kwa njia ya kawaida.
“Kwangu, Krismasi huanza na kanisa, kushukuru, ikifuatia na kuwazuru na kushiriki na wasiobahatika kupitia wakfu wangu – Mzazi Foundation. Nitashiriki muda mzuri na familia yangu pia,” akasema.
Sosholaiti Vera Sidika amechagua kuwa na muda na familia na kuzuru alikozaliwa, Kaunti ya Kakamega.
“Nitatumia muda na familia yangu – watoto wangu, mama na nyanya yangu,” anasema.
Mbunaji matini Kabi wa Jesus, anasema “tumechagua mpango wa nje ikiwemo ziara na watoto”.
Naye mwenzake Christine ‘Koku’ Lwanga anasema atashiriki muda na familia.
Mchekeshaji Mulamwah, anasema Krismasi inahusu watu.
“Mimi hutumia msimu huu kutangamana na familia na kukutana na jamaa na watu wapya katika familia zetu.”
Kwa mwimbaji wa Injili Daddy Owen, Desemba kwa kawaida huja na ratiba iliyojaa, isipokuwa mwaka huu.
“Naelekea kijijini, si kwa kazi, si kuonekana, lakini kwa familia,” anasema.
Napanga kunakili kila simulizi, kila jina, kila kumbukumbu, ili watoto wangu wasikue wakiwa wametenganishwa na historia.”
Ripoti za Elizabeth Ngigi na Esther Intabo