Habari

Natamani Rais wa kike – Uhuru

February 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amesifu mchango wa wanawake katika serikali yake na kusema kwamba anatamani kuona siku moja Kenya ikiongozwa na Rais mwanamke.

Akihutubia maskauti wanawake waliokusanyika Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi kuadhimisha Siku ya Kufikiria Ulimwenguni, Rais Kenyatta alisema wanawake wana vipawa vya uongozi na kwamba baadhi ya mawaziri wake wachapa-kazi ni wanawake.

“Ninaomba Mungu na ninatamani siku ambayo nitaketi na kusikiliza rais wa kwanza mwanamke akihutubia wananchi wa Jamhuri ya Kenya,” alisema Rais Kenyatta.

Alisema wanawake wanaelewa matatizo yanayokumba nchi na kujitolea kuchapa kazi ili kuyatatua.

Rais Uhuru Kenyatta ahutubu kwenye Kongamano la Kitaifa dhidi ya Ufisadi katika Ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi, Januari 2019. Picha/ Jeff Angote

“Baadhi ya mawaziri wangu wenye bidii ni wanawake. Wanawake wanaelewa maana ya kuwatumikia watu. Wanawake wanaelewa kujitolea kwa familia na nchi ambako ni muhimu kuliko mambo yote,” alisema.

Hafla hiyo iliyoandaliwa na mke wa Rais, Bi Margaret Kenyatta, ilihudhuriwa na zaidi ya maskauti wasichana 2,000 na viongozi wao kutoka kote nchini.

Waziri wa Elimu Bi Amina Mohamed na mwenzake wa Utumishi wa Umma Profesa Margaret Kobia pia walihudhuria.

Mawaziri wengine wanawake katika serikali ya Rais Kenyatta ni Bi Rychelle Omamo ( Ulinzi), Bi Sicily Kariuki ( Afya), Bi Faridah Karoney (Ardhi) na Dkt Monica Juma (Mashauri ya Kigeni).

Uwezo mkubwa

Rais Kenyatta alisema kwamba wanawake Wakenya; hasa vijana, wana uwezo mkubwa siku zijazo na wanafaa kutia bidii kila wakati ili kudhihirisha uwezo wao bila kukubali kushushwa na yeyote.

“Hakuna anayefaa kuwadharau eti kwa sababu wewe ni msichana kwa kisingizio kwamba huna uwezo,” alisema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa taifa alisema kwamba uongozi katika familia na nchi hauwezi kukamilika bila mchango wa wanawake.

“Kilicho muhimu ni kujitolea kwa familia na nchi. Nitaendelea kuunga mtoto wa kike na kuhakikisha kwamba amepata haki yake katika jamii yetu inayoitwa Kenya,” alisema.

Tangu Kenya ilipopata uhuru 1963, ni wanawake watatu tu waliowahi kugombea urais -Charity Ngilu (1997), Nazlin Umar (2007) na Bi Martha Karua (2013). Kwenye uchaguzi wa 2017, Bi Umar alizuiwa kugombea urais kwa kuwa hakuwa amesajiliwa kupiga kura.

Magavana wa kike na watatu pekee kati ya jumla ya magavana 47 nchini. Wao ni Ngilu ( Kitui), Joyce Laboso (Bomet) na Anne Waiguru (Kirinyaga).

Wanawake wamekuwa wakilalamika kuwa mazingira ya siasa nchini yanawapendelea wanaume zaidi. Kufikia sasa, bunge lililo na wabunge wengi wanaume limekataa kupitisha mswada wa jinsia kwamba thuluthi mbili ya wawakilishi hawafai kuwa wa jinsia moja.

Ijumaa, Bi Kenyatta aliwaambia wasichana hao waendelee kuwa imara, kudumisha heshima, maadili na uzalendo.

“Tunasherehekea wasichana na wanawake ambao wametoa nguvu na wakati wao kuwa maajenti wa mabadiliko,” alisema.
Aliwataja kama mashujaa na mfano mwema wa kuigwa na wote.