HATIMAYE Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro ametangaza kuwa hataunga mkono kuchaguliwa kwa Rais William Ruto kwa muhula wa pili mnamo 2027.

Mbunge huyo amefichua kuwa bado anathmini mrengo wa kisiasa unaorindima ngoma ya ‘Wantam’ atakaojiunga nao.

Akingumza kwenye mahojiano na NTV Ijumaa usiku, Bw Nyoro alikiri kuwa siasa ambazo zilihakikisha kuwa Rais William Ruto na UDA mamlakani zilikuwa zisizozingatia maadili.

“Tulipigana na watu na kuwaingilia kiasi cha kuwachafulia jina ili tushinde mamlaka. Zilikuwa siasa za ujinga. Wakati huo nilikuwa mdogo, sasa nina hekima,” akasema.

Alisema kuwa kuelekea mbele anataka kufahamika kwa siasa za ustaarabu, za hekima na zenye fikira kabla ya kuchukua hatua zozote za kisiasa
Wengi wamekuwa wakiuliza Bw Nyoro yupo katika mrengo upi kisiasa lakini sasa ameweka wazi kuwa hataki kuhusishwa na sera zozote za utawala wa Rais Ruto.

Aliwahakikishia Wakenya kuwa mrengo wa kisiasa atakaoungana ndio utakuwa unajali na utawatimizia maslahi yao kisiasa.

Hasa alifichua kuwa analenga kutanua mawanda yake na kushiriki siasa za kitaifa bila kuwasahau watu wa eneobunge lake la Kiharu.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí ambaye anaongoza Jubilee yake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ni kati ya viongozi ambao wapo upinzani na wameapa kuwa Rais Ruto atahudumu kwa muhula moja pekee.

Pia kuna tapo la viongozi wanaogemea mrengo wa Kenya Moja ambao wanaongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na baadhi ya viongozi waasi wa ODM.

“Si hekima kuanza kujiunga na miungano ya kisiasa mapema. Kuna miezi 20 kabla ya uchaguzi kufanyika na mambo yatabadilika,” akasema Bw Nyoro.

“Hivi vyama vyote unavyoviona havitafika 2027 vikiwa kwenye mirengo ya kisiasa vinavyoegemea kwa sasa. Mambo yatabadilika,”

Hata kama mambo yanatarajiwa kubadilika, Bw Nyoro alisema hawezi kuwa kwenye mrengo moja na Rais Ruto na uhusiano kati yao umesambaratika kiasi cha kutotengenea.

Alimkashifu Rais Ruto akisema ni kiongozi ambaye haaminiki na anaongoza serikali iliyolemewa kuwajibikia Wakenya na inavumilia sera mbaya.

“Alidanganya eti ananikuza kisiasa na kauli yake iliniudhi kwa sababu huo ndio wakati nilikuwa natimuliwa kama mwenyekiti wa kamati ya bajeti bungeni. Alikuwa ananikuza aje ilhali nilikuwa napokonywa wadhifa wangu?” akauliza.

Alikuwa akirejea kauli aliyotoa Rais Ruto mnamo Aprili 1 akiwa Ikulu ndogo ya Sagana ambapo alisema Bw Nyoro ni mwandani wake na angehakikisha anakwea ngazi kisiasa.

Alidai kuondolewa kwake kutoka kwa kamati hiyo ya hadhi kulitokana na uamuzi wa watu wa ngazi ya juu serikalini.

“Wandani wa rais walinivamia kwa maneno makali na kuonyesha walilenga kunipaka tope ili wanufaike kisiasa,” akasema.

Alifunguka na kusema alizungumza na Rais mara ya mwisho wakati ambapo bado alikuwa mwenyekiti wa kamati ya bajeti lakini hivi majuzi ameongea na Bw Gachagua.

“Bw Gachagua na mimi ni marafiki. Ndiyo tulikuwa na tofauti kati yetu alipokuwa naibu rais lakini bado sisi ni marafiki,” akasema.

Mbunge huyo anayehudumu muhula wake wa pili alisema kuwa hataki kushiriki siasa za kupaka tope familia za Bw Gachagua na Rais Ruto na siasa zake zitajikita kwenye masuala ya kuleta uongozi bora kwa Wakenya.

Alipoulizwa kwa nini anapinga sera za sasa ilhali ziliasisiwa alipokuwa mwenyekiti wa bajeti, Bw Nyoro alijitetea vikali na kujitenga na sera za sasa akisema hazipeleki nchi mahala popote.

Alikariri kwamba alipinga mikopo ya kiholela, makato ya Wakenya kutumika kuboresha miundomsingi, kuuzwa kwa mashirika ya serikali na karo ya shule kupandishwa.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Murangá Mixson Warui, Bw Nyoro sasa anazungumza lugha ya wakazi wa Mlima Kenya ambao hawataki uongozi wa Rais Ruto.

“Anajihusisha na maoni ya wengi lakini bado anachukua muda wake kusoma mwelekeo wa kisiasa ili aingie ule ambao utamfaa na kukweza ndoto zake za kisiasa,” akasema Bw Warui.