Familia yalilia haki baada ya mwanao kuuawa mikononi mwa DCI
FAMILIA ya mshukiwa wa wizi Sylvester Mwenda inalilia haki kwa kupatikana ameaga dunia siku tatu baada ya kunyakwa na watu waliojitambulisha kama polisi nyumbani kwake Kinna-Meru, Kaunti ya Meru.
Kwa mujibu wa mjane wake Glory Gatwiri, wanaume walionyaka Mwenda,30 walijitambulisha kama polisi kutoka Idara ya Upelelezi Nchini (DCI). Walimnyaka na kuondoka na gari lake aina ya Toyota Probox.
Mnamo Jumanne Afisa wa Uchunguzi wa Uhalifu (CCIO), Abednego Kavoo alithibitisha Mwenda alikamatwa akidaiwa kuhusika na misururu ya visa vya wizi maeneo ya Igembe na Tigania.
Hata hivyo, Disemba 22, badala ya kufikishwa kortini pamoja na washukiwa wengine, mwili wa Mwenda ulipatikana katika makafani ya Hospitali ya Nyambene Level Four baada ya majaribio kadhaa ya kupata maelezo kutoka kwa polisi kufeli.
“Walipokuja nyumbani kwetu Ijumaa iliyopita walijitambulisha kama maafisa wa DCI kutoka Maua ila hawakutuambia kosa ambalo Mwenda alikuwa amefanya. Jumamosi nilimtembelea katika kituo cha polisi cha Maua lakini sikuweza kuongea naye,” akasema Bi Gatwiri.
Alisema kuwa baadaye Jumamosi hiyo, makachero hao waliandamana na Mwenda hadi shamba lake Kinna-Meru.
“Wakiwa hapo walimnyaka rafikiye Mwenda ambaye ni polisi wa akiba. Waliwachukua mbuzi wetu wanne wakisema walikuwa wa kusherehekea Krismasi. Mwendwa alionekana kama mtu aliyeteswa, akapigwa vibaya na kujeruhiwa,” akasema.
Baada ya kukosa kuwasilishwa Mahakama ya Maua Jumatatu walienda vituo vya polisi vya Maua na Mutuati lakini wakaambiwa hakuwa huko.
Walipiga ripoti katika kituo hicho hicho cha Maua na kupewa OB nambari 70/22/12/2025.
Shemejiye Mwendwa Richard Kamencu alisema kuwa baadaye waligundua kuwa mwili ulipelekwa kwenye makafani ya Nyambene Jumamosi usiku.
“Mhudumu wa mochari alituambia mwili huo ulipelekwa na polisi ambao walisema aliuawa na umati. Aliuawa aje na umati ilhali alikuwa akizuiliwa na polisi?” akauliza Bw Kamencu.
Bw Kavoo hata hivyo anasema Mwenda alivamiwa na kuuawa na umati Kinna-Meru saa 12 Jumamosi akiwaongoza makachero kuwatambua washukiwa zaidi.