MKEWE mwanasiasa Cyrus Jirongo, Anne Lanaoi jana alisema kuwa mumewe alimwaarifu kuwa angekutana na Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangúla siku ambayo aliaga dunia huku wito ukizidi kutolewa kuhusu uchunguzi wa kina kuhusu kifo cha waziri huyo wa zamani.

Mwanasiasa huyo nguli ambaye alihudumu kama mbunge wa Lugari, aliaga dunia mnamo Disemba 13, Karai, Naivasha kwenye barabara ya Nakuru-Nairobi.

Gari lake linadaiwa liligonga na basi la Climax lililokuwa likielekea Busia.

Jana ibada ya kumuenzi marehemu iliandaliwa katika Kanisa la Citam Valley Road ambapo watoto 21 na wake watatu wa marehemu waliungana na wanasiasa kuombea roho yake kabla ya mazishi yake Disemba 30 Lugari.

Wakati wa ibada hiyo, Bi Lanaoi alisimulia matukio ya mchana wa Disemba 12 siku moja kabla ya mauti yaliyompata marehemu mumewe.

Alisimulia kuwa mnamo Disemba 12, Bw Jirongo alimpigia na kutaka kufahamu alikokuwa.

“Nilimwambia nilikuwa kwenye Supamaketi na alitaka kuniona. Aliendesha gari hadi mahali nilikuwa kisha nikaweka toroli kando na nikaenda kumwona,” akasema

Wakati wa mazungumzo yao ndani ya waligusia masuala ya ndani ya kibiashara na walipomaliza mumewe alimwambia anarudi ofisini kushughulikia kazi zake.

Pia ni wakati huo alimfichulia kuhusu mipango yake ikiwemo mkutano na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla.

Akionekana mwenye huzuni nyingi, alisema kuwa Bw Jirongo hakumwaambia chochote kuhusu kuelekea Naivasha na alipigwa na butwaa kuhusu ajali iliyompata huko.

“Baadaye alinipigia saa 10 jioni akaniambia hakuenda afisini na alikuwa amelala tu kwa kiti kwa muda wa saa mbili,” akasema.

Hakufahamu kuwa kukutana na Bw Jirongo kwenye maegesho ndiko kulikuwa mara ya mwisho alikuwa akimwona mumewe.

Alisimulia kuwa baada ya kikao na Bw Jirongo aliingiwa na wasiwasi wala hakutulia, akisema kifo cha mumewe kimekuwa pigo sana kwake.

Kinara wa PLP Martha Karua alifichua kuwa Bw Jirongo alikuwa ameashiria alipanga  kuimarisha usalama wake.

“Alikuwa na wasiwasi kuhusu usalama wake na alitaka kuumarisha. Ajali hii ilikuja kabla ya wakati huo na maswali mengi sasa yanazuka,” akasema Bi Karua.

Naye Seneta wa zamani wa Vihiga George Khaniri, rafikiye marehemu alisema haamini Bw Jirongo aliendesha gari kivyake hadi Naivasha.

“Katika hali aliyokuwa, nasema hangeweza kuendesha gari hadi Naivasha. Kuna mianya mingi na sijaona hata abiria mmoja aliokuwa kwenye basi akijitokeza na kusema alishuhudia ajali hiyo,” akasema Bw Khaniri.