• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
CHOCHEO: Uwezo wa kuzaa wapungua, kunani?

CHOCHEO: Uwezo wa kuzaa wapungua, kunani?

Na BENSON MATHEKA

UNAFAA kujiandaa kupata watoto mapema iwezekanavyo maishani kwa sababu uwezo wa wanawake kuzaa unaendelea kupungua.

Wataalamu wanasema miaka ya mwanamke kukosa kupata hedhi na hivyo kumfanya kutopata mimba imepungua mno.

Wanasema kwamba kwa baadhi ya wanawake, uwezo wa kupata mimba huanza kutoweka wakiwa na umri wa miaka 30.

“Kuanzia miaka 30, mwanamke anaweza kuanza kupata dalili za kusitisha hedhi. Kwa kawaida, hizi huwa ni dalili za kupungua kwa uwezo wa mwanamke kupata mimba,” asema mtaalamu wa afya ya uzazi Nannete Satori kwenye makala yaliyochapishwa mtandaoni.

Kulingana na Nannete, dalili nyingi za mwili kukoma hedhi huanza mtu akiwa na miaka 30, kipindi ambacho kinafahamika kama perimenopause.

Dkt Patricia Wendo, mtaalamu wa afya ya uzazi katika hospitali ya Penda jijini Nairobi anasema ni kipindi ambacho mtu huanza kupata mabadiliko katika mfumo wao wa hedhi.

Anasema mwanamke akikosa kupata hedhi kwa miezi 12, mwili huwa umeingia katika kipindi cha kutoweza kupata watoto. Kulingana na Nanette, hali hii huanza kwa kuruka mwezi au miezi bila kupata hedhi. ?Pia huanza taratibu na wengi huichukulia kama ya kawaida.

“Huwa inaanza polepole na watu wengi huichukulia kama mabadiliko ya kawaida. Japo kuna mambo mengi yanayochangia mwili wa mwanamke kutopata hedhi kila mwezi, kuna haja ya mtu kuwa mwangalifu ili asikose kupata watoto hali hiyo ikimpata mapema,” asema Dkt Wendo.

Hata hivyo, anasema mtu akikosa kupata hedhi akiwa kati ya umri wa miaka 30 na 45, anafaa kupimwa mimba kwanza kabla ya kuchukulia kwamba mwili wake umeingia awamu ya kukoma kutoa hedhi.

“Kwa watu walio na miaka 30 na chini ya 45, kukoma hedhi kunaweza kuchangiwa na mambo mengine kama vile kupata mimba. Ni muhimu kuthibitisha hawana ujauzito kabla ya kuamini kwamba wameanza kipindi cha mwili kukosa uwezo wa kupata mimba,” aeleza.

Miaka kumi

Wataalamu wanasema kipindi hiki kinaweza kudumu hata miaka kumi. Wakati wa kipindi hicho, mtu huwa anahisi dalili wanazopata wanawake ambao mili yao imekoma kabisa kupata hedhi.

“Mwili hupata joto jingi na jasho ambalo huwa linaenea hadi usoni. Dalili hizi zikipata mtu usiku, huwa anatatizika kupata usingizi,” aeleza Dkt Wendo.

“Mwanamke akianza kupata hali hii, pia huwa anaanza kuwa mwingi wa hasira na baadhi ya wanawake hupata mfadhaiko,” aongeza. Wataalamu wanasema kwamba wakati huu, wanawake hutatizika kupata usingizi na hata kauka kwa uke. Hali hii, aeleza Dkt Wendo, huwa inasababishwa na kupungua kwa viwango vya homoni mwilini.

Dkt Nanette anasema hali hii inaweza kuwa ya kurithi au kuchangiwa na mitindo ya maisha.

“Iwapo mwili wa mama yako ulikoma hedhi mapema na mtindo wako wa maisha ni sawa na wake, kuna uwezekano ukapatwa na hali sawa,” aeleza Dkt Wendo.

Anawashauri wanawake kuacha kuvuta sigara na kulewa akisema huwa kunawafanya kufika awamu hii mapema na kuwanyima uwezo wa kupata mimba. Anasema mtu akipata dalili hizi anafaa kumuona mtaalamu wa afya ili apate ushauri.

“Kujadili hali hii na mtaalamu wa afya kunasaidia sana badala ya kusononeka pekee,” asema.

Anaeleza kuwa ushauri wa wataalamu unaweza kumsaidia mtu kujipanga kimaisha na hasa kuhusu watoto anaotaka kuzaa.

You can share this post!

Natamani Rais wa kike – Uhuru

Spurs, Palace ni kijasho ligi ya EPL

adminleo