Habari za Kitaifa

Upinzani ukiweka kura zao kapu moja utamlemea Ruto, uchambuzi wa utafiti wabaini

Na EDWIN MUTAI December 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto angepata asilimia 28 ya kura iwapo uchaguzi mkuu ungeandaliwa leo, utafiti mpya uliofanywa na kampuni ya Infotrak umeonyesha.

Hata hivyo, uchambuzi unaonyesha kwamba iwapo wanasiasa wanaoegemea mrengo wa United Opposition wangeweka kura zao katika kapu moja, basi wanaweza kumpa Rais wakati mgumu kujipatia muhula wa pili.

Utafiti huo unaonyesha kuwa Rais Ruto atashinda wingi wa kura lakini hatapata asilimia 50 na kura moja inayotakikana kikatiba ili ashinde duru ya kwanza.

Anafuatwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kwa asilimia 13 kisha Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka kwa asilimia 12.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ana asilimia saba, Kiongozi wa PLP Martha Karua asilimia mbili sawa na Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga.

Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, mwenzake wa Trans Nzoia George Natembeya na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro wana asilimia moja huku George Wajackoyah na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wakitoshana kwa asilimia 0.2.

Ripoti ya utafiti huo inaonyesha asilimia 27 ya Wakenya bado hawajaamua ni nani watampigia kura za urais 2027.

Utafiti huo ulifanywa kati ya Desemba 19 na 20, 2025 ambapo watu 1,000 walihojiwa. Infotrak inasema waliohojiwa ni Wakenya wanaozidi umri wa miaka 18.

SOMA PIA: Ruto aongoza kwa umaarufu wa wawaniaji urais kura za 2027 – Utafiti

“Muundo wa utafiti huu uliafikiwa kwa kutumia takwimu za sensa ya 2019. Kuna pengo la usahihi la asilimia tatu, na matokeo ya utafiti huu yanaaminika kwa asilimia 95,” ikasema ripoti hiyo.

“Utafiti huo ulifanyika kwenye kaunti 47 na kanda nane za Kenya. Kuhakikisha usawa wa kitaifa, ulifanywa maeneo yote.”

Kuhusu umaarufu wa Vyama vya Kisiasa, UDA ya Rais Ruto ina asilimia 23 huku ikifuatwa na ODM kwa asilimia 19.

Hii ndiyo mara ya kwanza UDA kuipita ODM kwa umaarufu. Vyama hivyo vilikuwa nguvu sawa kwa asilimia 16 kwenye utafiti uliofanywa mnamo Agosti.

Kwenye utafiti uliofanywa Septemba na Julai 2024, ODM ilikuwa na umaarufu wa 38-16 dhidi ya UDA na 34-17 mtawalia.

Jubilee inayoongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ina asilimia nne huku Wiper ikiwa na asilimia sita, sawa na DCP ya Bw Rigathi Gachagua.

Iwapo uchaguzi ungeandaliwa leo, Rais angepata asilimia 76 ya kura za Kaskazini Mashariki kisha Bonde la Ufa apate asilimia 42, Nyanza (asilimia 30), Pwani (asilimia 23), Mashariki (asilimia 17), Nairobi (asilimia 16) na Kati (asilimia 14).

Dkt Matiang’i angepata asilimia 18 Nyanza, Bonde la Ufa (asilimia 17), Mashariki (asilimia 16), Magharibi (asilimia 15), Nairobi (asilimia 11), asilimia 10 Pwani na 0 Kaskazini Mashariki.

Bw Musyoka angepata asilimia 20 Mashariki, Nairobi (asilimia 17), Pwani na Magharibi ni asilimia 11 kisha apate asilimia 10 Bonde la Ufa, Nyanza (asilimia 9), Kati (8) na Kaskazini Mashariki (2).

Utafiti huo, aidha, ulionyesha kuwa asilimia 32 ya wapigakura wanaunga mkono Serikali Jumuishi. Ni asilimia 22 wanaounga muungano wa upinzani unaoongozwa na Bw Musyoka, Gachagua, Matiang’i, na Kinara wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa.

Kenya Moja inayohusishwa na Gavana Natembeya na Seneta Sifuna, Babu Owino, Bi Gathoni wa Muchomba na Bw Nyoro ina asilimia 17. Wale ambao hawaungi mrengo wowote wa kisiasa ni asilimia 29.

Serikali Jumuishi inashabikiwa Kaskazini Mashariki zaidi kwa asilimia 88, Bonde la Ufa (asilimia 39), Nyanza (asilimia 38), Pwani (asilimia 36), Magharibi (asilimia 31), Mashariki (asilimia 23), Nairobi (asilimia 16), kisha Kati (asilimia 13).

Upinzani nao una ufuasi mkubwa eneo la Kati kwa asilimia 31, Mashariki (asilimia 36), Nairobi (asilimia 25), Pwani (asilimia 20), Bonde la Ufa na Magharibi (asilimia 13) na Nyanza asilimia tisa.

Kenya Moja inaungwa mkono sana Nyanza kwa asilimia 26, Nairobi (asilimia 25), Bonde la Ufa na Magharibi (asilimia 18), Mashariki (asilimia 14), Pwani (asilimia 13) kisha Kaskazini Mashariki (asilimia mbili).

Eneo la Kati lina idadi ya juu ya Wakenya ambao hawaungi mkono mrengo wowote wa kisiasa kwa asilimia 36, Magharibi (asilimia 35), Nairobi (asilimia 34), Pwani (asilimia 30), Mashariki (asilimia 27), Bonde la Ufa (asilimia 26) kisha Kaskazini Mashariki kwa asilimia 10.

Gharama ya maisha (asilimia 46), ufisadi (asilimia 27), Afya (asilimia 27), elimu (asilimia 26), ukosefu wa ajira (asilimia 25), uongozi wenye maadili (asilimia 23), usimamizi wa kiuchumi (asilimia 21), usalama (asilimia 16), ugatuzi (asilimia 11) na nyumba za gharama nafuu (asilimia tatu) ndizo zitatumiwa na wapigakura kuamua kiongozi watakayemchagua 2027.