MAONI: Viongozi wagawe vyakula wakati wa majanga pia, si Krismasi tu
KIPINDI cha Krismasi ni wakati ambapo familia nyingi hujumuika pamoja na kushiriki vyakula na vinywaji kama njia moja ya kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristu, ambaye Wakristu humwamini kuwa mwokozi wao.
Katika sherehe za mwaka huu, takribani kila sehemu ya nchi, wanasiasa au viongozi wanaoshikilia nyadhifa kuu serikalini walionekana wakigawa vyakula kwa raia kama njia moja ya kuwatakia Krismasi njema.
Walipokuwa wakitoa vyakula hivyo vilivyojumuisha bidhaa kama vile unga wa ngano, mchele, mafuta ya kukaangia na vinginevyo, wanasiasa hao walihakikisha kuwa wanapiga picha za matukio hayo na kuzisambaza katika mitandao yao ya kijamii kama njia moja ya kujipiga kifua kuwa wametoa.
Waswahili husema kutoa ni moyo wala si utajiri. Lakini katika matukio tuliyoyashuhudia msimu huu wa Krismasi, utoaji wa misaada hiyo ni dhihirisho tosha jinsi wanasiasa wanavyotumia ufukara wa raia ili kuwavutia wawapigie kura kunapotokea uchaguzi.
Nilipokuwa nikitazama picha walizoziweka mitandaoni, swali moja lilinijia akilini; mbona panapotokea majanga inakuwa nadra kwa wanasiasa hao kutoa misaada kama hiyo?
Nitatolea mfano msukosuko wa kikabila unaoendelea katika eneo la Angata Barikkoi, Trans Mara katika Kaunti ya Narok.
Vita hivyo baina ya jamii tatu vimesababisha raia wengi kuchomewa makazi yao na mali ya thamani kubwa kuharibiwa. Isitoshe, angalau watu wanne wamefariki kutokana na uhasama huo.
Kwa kuhofia maisha yao, raia hao wamekuwa wakikita kambi katika shule na vituo vya polisi vya eneo hilo.
Katika mahojiano mengi ambayo waathiriwa hao wamefanyiwa, wanalia kuhusu ukosefu wa chakula na vifaa vingine muhimu vya kutumia kama vile magodoro na mablanketi ya kujifunika ili wajikinge kutokana na baridi kali inayowang’ata nyakati za usiku.
Katika kambi hizo, kina mama, watoto na watu wenye ulemavu ndio wameathirika zaidi.
Wamekuwa wakitoa wito kwa serikali na watu wengine kuwasaidia lakini misaada hiyo haijakuwa ikitolewa kwa fujo jinsi tumeshuhudia wakati wa Krismasi.
Kwa hivyo ni maoni yangu kuwa, wanasiasa na viongozi wa serikali wanafaa kutoa misaada kama waliyotoa kwa wingi wakati wa Krismasi kwa waathiriwa kama wa Trans Mara.
Haifurahishi hata kidogo unapowatazama waathiriwa hao wakilia katika runinga na vyombo vingine vya habari wakilalamikia kile wanachosema ni kutelekezwa na serikali ambayo inafaa kuwashughulikia.
Si kwa raia hao wa Trans Mara tu, hata kunapotokea mafuriko na gharika, Wakenya wanaoishi katika nyanda za chini hutaabika kupata vyakula na vifaa vingine vya kujimudu.
Kutoa misaada kwa waathiriwa wa majanga, kwa maoni yangu, ni majukwaa mazuri ya wanasiasa kujijenga na kuimarisha uungwaji mkono wao na wala si Krismasi tu.
Kutoa misaada kwa watu walioathirika na majanga ndio njia pekee ya kuonyesha kwa kweli anayetoa ana nia njema na si kujinufaisha kisiasa.
Ikiwa tutawakumbuka watu walio katika majanga kama hayo, basi nina imani kuwa kama taifa tutasonga mbele.