Kocha McCarthy alivyoleta matumaini tele, mwamko mpya katika soka ya Kenya
KOCHA Benni McCarthy aliandika historia mapema mwezi huu, kwa kuwa kocha wa kwanza wa kigeni wa Harambee Stars kutuzwa na Serikali.
Raia huyo wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 48, alikuwa miongoni mwa mamia ya watu waliopewa heshima mbalimbali na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi baada ya sherehe za Siku ya Jamhuri zilizofanyika katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi.
McCarthy, mshambuliaji wa zamani wa West Ham United na Blackburn Rovers, na kocha wa washambuliaji wa kikosi cha kwanza cha Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), alitunukiwa Tuzo ya Rais (HSC – Kitengo cha Raia).
Utambuzi huo ulitokana na kikosi cha Stars kufanya vizuri katika michuano ya Mataifa ya Afrika ya Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024.
Kenya ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya mataifa 19 yanayofanyika kila baada ya miaka miwili, pamoja na Uganda na Tanzania kuanzia Agosti 2 hadi 30 mwaka huu.
Wakishiriki CHAN kwa mara ya kwanza katika historia, na wakiwa wamepangwa katika kile kinachoweza kuitwa ‘Kundi la Kifo’, Wakenya wengi hawakuwa na matarajio yoyote kutoka kwa Stars hata kabla ya mashindano kuanza.
Vigogo Morocco, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Angola na Zambia walikuwa pamoja na Stars kwenye michuano hiyo.
Shaka kutoka kwa Wakenya pia ilitokana na matokeo duni ya Stars katika mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026.
Kinaya ni kuwa Kenya iliongoza kundi hilo, kabla ya kuondolewa katika robo-fainali na Madagascar. McCarty alipokea sifa tele baada ya kufufua soka ya Kenya.
Wakicheza mbele ya maelfu ya mashabiki katika uwanja wa MISC Kasarani, vijana hao wa nyumbani waliwashangaza Morocco na DRC kwa kuwafunga 1-0 na kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Angola.
Kwa kushangaza, Stars walicheza zaidi ya saa moja wakiwa na wachezaji 10 dhidi ya Morocco na Angola kufuatia kadi nyekundu kwa viungo Marvine Nabwire na Chrispine Erambo mtawalia.
Kenya ilihitimisha kampeni yao ya kundi kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Zambia, kabla ya kupoteza 4-3 kwa Madagascar katika mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa kawaida.
Baada ya kufunga bao pekee katika ushindi wa Kenya dhidi ya DRC, kiungo Austine Odhiambo aliongeza idadi yake kwa kusawazisha bao la wenyeji kutokana na penalti katika sare yao dhidi ya Angola.
Mshambuliaji Ryan Ogam alifunga mabao ya pekee katika ushindi wa Kenya dhidi ya Morocco na Zambia huku beki Alphonce Omija akifunga katika sare ya Stars dhidi ya Madagascar katika raundi ya nane bora.
Keny,a ambayo haikupoteza katika mechi za hatua ya makundi, iliongoza Kundi A ikiwa na pointi 10 ikifuatiwa na Morocco kwa alama tisa.
DRC ilimaliza ya tatu na alama sita huku Angola na Zambia zikifuata kwa pointi nne na sufuri mtawalia.
McCarthy alishinda taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) akiwa na klabu ya Ureno ya FC Porto mnamo 2004. Alizinduliwa kama kocha wa Stars mnamo Machi 3 kwa mkataba wa miaka miwili.
Waliojiunga naye ni pamoja na Vasili Manousakis (kocha msaidizi), Moeneeb Josephs (kocha wa makipa) na Pilela Maposa (mtaalamu wa matokeo).
Baada ya Harambee Stars kushikilia ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Morocco licha ya kucheza zaidi ya saa moja wakiwa na wachezaji 10 kufuatia kadi nyekundu kwa Erambo, McCarthy alieleza kuwa, kuzuia kutofungwa katika mechi hiyo kulitokana na mbinu alizojifunza Porto chini ya kocha Jose Mourinho.
“Sina hakika mnakumbuka kuwa nilicheza chini ya kocha fulani, Jose Mourinho. Alikuwa bingwa wa hilo, kwa hivyo kama mchezaji, kucheza katika timu inayocheza na wachezaji 10 ilikuwa ngumu sana, lakini tulikuwa tukifanikiwa kikamilifu kwa kuwa lilikuwa jambo letu la kila siku,” alisema.
Zaidi ya uwezo wake wa kimbinu, McCarthy pia alionyesha kuwa haogopi. Katika mechi zote nne za Kenya kundini, kocha huyo wa zamani wa Cape Town City FC na AmaZulu FC alifanya mabadiliko kadhaa katika kikosi chake cha kwanza, ambayo mara nyingi yalizaa matunda.
Mfano mmoja ulikuwa katika mechi dhidi ya Morocco ambapo alipumzisha wachezaji wake kadhaa muhimu akiwemo nahodha Abud Omar, Odhiambo, Omija, Daniel Sakari, Alpha Onyango na Nabwire. Baadhi ya nafasi zao zilijazwa na mabeki Lewis Bandi, Siraj Mohamed na Michael Kibwage na mshambuliaji Ogam.
Kenya iliwakatisha tamaa Morocco katika mechi nzima, huku Ogam akifunga bao la ushindi. McCarthy kisha alieleza kuwa hatua nzuri ya timu yake katika mashindano hayo ilitokana na uhusiano mzuri waliokuwa wameunda kati yao. Pia alitaja sapoti kubwa ya mashabiki.
“Sidhani tungefanya vizuri bila mashabiki. Walikuwepo nasi wakati wachezaji walicheza 10 na hata 11,” alisema kocha huyo baada ya ushindi wao dhidi ya Morocco.
Ushindi wa Kenya pia ulitokana na ahadi ya Rais William Ruto kuwatuza Stars. Kwa kila ushindi, Rais Ruto alimzawidi kila mtu wa kikosi cha Stars Sh1 milioni huku kila mmoja kikosini akipata Sh500,000 kwa matokeo sare.
Kuelekea mechi ya mwisho ya kundi la Kenya dhidi ya Zambia, Rais Ruto aliongeza dau kwa kuahidi kila mmoja katika timu Sh2.5 milioni ikiwa watashinda mechi hiyo. Kwa jumla, kila mchezaji alipokea Sh5 milioni kutoka kwa Rais.
Hata hivyo, McCarthy katika siku za hivi karibuni amekosolewa kutokana na matokeo duni ya Stars. Baada ya CHAN, Kenya ilielekeza mawazo kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 Kundi F ambapo ilicheza hata ingawa matumaini ya kufuzu yalikuwa yamefifia.
Kenya ilipoteza 3-1 dhidi ya Gambia mwezi Septemba kabla ya kunyorosha Ushelisheli 5-0. Stars ilijibu dhidi ya Burundi kwa ushindi wa 1-0 kabla ya kupoteza 3-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika, Ivory Coast.
Mwezi uliopita, Kenya ilipoteza 1-0 dhidi ya Equatorial Guinea, na 8-0 dhidi ya Senegal katika mechi za kirafiki nchini Uturuki.
Kipigo kikubwa dhidi ya Senegal kilizua ukosoaji mkali kutoka kwa mashabiki, kwani ni miongoni mwa vipigo vikubwa zaidi katika historia ya soka ya Kenya.
Hata hivyo, baadhi ya washikadau walitetea McCarthy, wakisema, Senegal ni nguvu ya soka na kwamba walichezesha kikosi kamili katika mechi hiyo ikiwa ni pamoja na wazoefu kama Sadio Mane, Nicolas Jackson na Kalidou Koulibaly.
Katika mechi za baada ya CHAN, McCarthy amewapa fursa wachezaji chipukizi kuonyesha talanta zao. Alisema ni kwa maandalizi ya AFCON 2027 ambapo Kenya itakuwa mwenyeji mwenza na Uganda na Tanzania.
Job Ochieng wa Real Sociedad, Bryton Onyona wa Gor Mahia, Vincent Harper (Walsall, England), Adam Wilson (The New Saints, England) na Kevin Otiende (Nairobi United) ni baadhi ya sura mpya ambazo zimepewa fursa ya kuonyesha uwezo wao ugani.
Baada ya kushindwa kufuzu kwa AFCON inayoendelea nchini Morocco na Kombe la Dunia la 2026, McCarthy anatarajiwa kuelekeza nguvu zake kikamilifu katika kuandaa kikosi chake kwa AFCON 2027.