Habari za Kitaifa

Majirani wa Ruto wahangaikia chakula, matibabu na makazi mzozo wa ardhi ukikolea Narok

December 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ILIPOBAINIKA kuwa Rais William Ruto alikuwa amenunua shamba la Murumbi, Kilgoris na kuhamia eneo hilo, wakazi wengi wa Ang’ata Barikkoi, Trans Mara, walifurahia sana.

Ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 uliwapa furaha zaidi, kwani walihisi mmoja wao sasa alikuwa amefika katika kilele cha uongozi wa taifa.

Waliamini methali “mgeni njoo, mwenyeji apone,” ingekuwa kweli.

Walitarajia kumalizika kwa mapigano ya kikabila yaliyokuwa yakitokea kila mara, pamoja na kuimarika kwa usalama, amani na maendeleo.

Hata hivyo, matumaini hayo yalibaki ndoto tu. Miaka miwili iliyopita imekuwa ya mateso makubwa kwa wakazi hao, huku mapigano ya kikabila yakiwanyima amani, usalama na maendeleo.

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita pekee, mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua wanne, makumi kujeruhiwa na zaidi ya watu 1,800 kulazimika kuhama makazi yao.

Haya yote yanatokea licha ya Rais Ruto kufanya nyumba yake ya Kilgoris kuwa kituo cha mikutano mbalimbali.

Kwa kawaida, uwepo wa Rais ungetarajiwa kuleta nafuu kwa jirani zake.

Hata hivyo, kwa wakazi wa Ang’ata Barikkoi, takriban kilomita 35 kutoka Kilgoris, mateso yamekuwa ndiyo maisha ya kila siku, huku mapigano yakiongezeka katika mwaka uliopita.

Dkt Ruto ametumia msimu huu wa sherehe nyumbani kwake Kilgoris, lakini jirani zake wa Ang’ata Barikkoi hawana cha kusherehekea.

Wanasema mwaka wa 2025 umekuwa mbaya zaidi kwao wala hawaoni dalili za 2026 kuwa bora, hasa baada ya kulazimika kuhama makazi yao kutokana na mapigano yaliyozuka tena mwezi mmoja uliopita.

Familia zilizohamishwa zinaishi kwa taabu baada ya kukimbia makazi yao kwa sababu ya ukosefu wa usalama. Hakuna msaada wowote wa serikali unaoonekana, huku shule zikitarajiwa kufunguliwa mapema wiki hii.

Hali ya familia zinazohifadhiwa katika Shule ya Msingi ya Sankale ni mbaya. Umepita mwezi mmoja tangu walipokimbia makazi yao kutokana na mapigano yanayoendelea, na wanasema hawajapokea msaada wowote kutoka kwa serikali ya kitaifa -iwe ni chakula au msaada wa kuwarejesha nyumbani.

Ukosefu wa msaada huo umeacha familia hizi katika hali ya suitafahamu na kutamauka. Bw David Kirui, anayewakilisha familia zilizoathiriwa, alieleza masikitiko yake akisema wamekuwa wakitegemea misaada kutoka Kanisa Katoliki na Shirika la Msalaba Mwekundu.

“Tumeshtuka kuona viongozi wetu hawajatujulia hali wala kutupa msaada wowote,” akasema.

“Tumeachwa kujitegemea bila kujua ni lini tutarudi nyumbani au kupata msaada.”

Mirriam Koros, mama wa pacha wachanga, alizungumza kwa hisia kuhusu hali yake ngumu.

“Mimi na watoto wangu tunalala sakafuni darasani, bila mahitaji ya msingi kama chakula cha kutosha, maji na vyoo. Nina hofu watoto wangu wanaweza kuugua, labda nimonia, kutokana na baridi kali usiku. Ninataka tu mahali salama pa kuishi na watoto wangu, lakini inaonekana hakuna anayesikia kilio chetu,” akasema.

Kanisa Katoliki limekuwa likitoa msaada wa nguo na chakula.

Padri Felix Ndolo, ambaye amekuwa mstari wa mbele kusaidia familia hizo, alitoa wito kwa serikali kuingilia kati haraka.

“Hali inazidi kuwa mbaya kila siku, na inavunja moyo kuona familia, hasa watoto, wakiteseka hivi,” alisema.

Alihimiza pia jamii zote za Trans Mara kuishi kwa amani, akisisitiza kuwa amani ndiyo njia pekee ya kuinua taifa.

“Tuweke kando tofauti zetu na tufanye kazi pamoja kwa ajili ya amani. Amani ndiyo njia pekee ya kujenga taifa,” aliongeza.

Familia zilizofurushwa makwao zimeomba serikali na mashirika ya kibinadamu kuwasaidia kwa chakula, makazi na huduma za matibabu.

Pia zimetoa wito kwa serikali kuharakisha juhudi za kutatua mzozo huo na kuhakikisha wanarejea makwao kwa usalama.

Kadri siku zinavyosonga, hali ya familia hizo inaendelea kuzorota, na kufanya haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kuwa ya dharura zaidi.

Akizungumzia mapigano hayo hivi majuzi, Rais Ruto aliwaamuru wakazi walio na silaha haramu kuzisalimisha mara moja kwa polisi.

Rais aliahidi kurejesha utulivu akisema: “Silaha lazima zirudishwe kwa polisi. Wasipofanya hivyo, watakabiliwa vikali kisheria. Lazima tukomeshe wahalifu, magaidi na wote wanaovuruga amani na usalama wa wananchi wengine.”

Ingawa mzozo huo umehusishwa na mgogoro wa ardhi, watu wenye ushawishi wanaripotiwa kutumia hali hiyo kuchochea ghasia.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen ameidhinisha msako wa siku 30, akitaja maeneo 14 kuwa hatari.

Katika Trans Mara Magharibi, eneo la Nkararo limetajwa.

Trans Mara Kusini, maeneo 13 yametajwa, yakiwemo Oldonyo-Orok, Siteti, Ololoma, Corner, Ratiki, Isokon, Kerinkani, Kondamet, Olkiloriti, Ang’ata Barikkoi, Kapkures, mji wa Lolgorian na Mashangwa.