Baraza la Makanisa lahimiza vijana kujipanga mtandaoni kuelekea 2027
BARAZA la Makanisa Kenya (NCCK), linawahimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kuungana kisiasa kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Mwenyekiti wa kitaifa wa NCCK, Askofu Dkt Elias Otieno Agola, alisema hatua kama hiyo itaunda mustakabali wa Kenya.
“Mwaka wa 2026, vijana wanapaswa kutumia mitandao ya kijamii kuandaa na kuwasilisha wagombeaji vijana kwa nyadhifa zote za kuchaguliwa. Ushiriki wa kisiasa unaofaa na wa kimaadili leo utatoa uongozi wenye uwajibikaji kesho,” alisema Dkt Otieno.
Kauli hiyo ilitolewa kama sehemu ya taarifa yake ya mwisho wa mwaka yenye mada “2026 Mwaka wa Tumaini na Ahadi ya Amani.”
Askofu Otieno alisisitiza kuwa vijana ndio moyo na mustakabali wa taifa, akiwahimiza kujisajili kama wapigakura na kushiriki katika asasi rasmi za utawala ikiwemo vyama vya kisiasa.
Wapiga kura wenye umri wa 18–35 wanatarajiwa kuwa kundi kubwa linaloweza kuamua matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 jambo ambalo linaonyesha nguvu ya vijana kubadilisha siasa nchini.