Habari

Wafugaji Baringo walia kutofaidi mnada wa mbuzi wa Kimalel

Na CECIL ODONGO December 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAFUGAJI wa mbuzi katika Kaunti ya Baringo wamelalamika kwamba walilaghaiwa na maafisa wa serikali ya kaunti wakati wa Mnada maarufu wa Mbuzi uliofanyika majuzi katika eneo la Kimalel eneo bunge la Baringo Kusini.

Baadhi yao walielezea kuvunjwa moyo baada ya mbuzi wao kukataliwa kwa madai hawakutimiza “viwango hitajika” katika mnada huo maarufu ulioanzishwa na rais wa zamani, Hayati Daniel Moi mnamo 1986 kwa ajili ya kuwainua wafugaji kiuchumi.

Mmoja wa wafugaji, alilalama kuwa maafisa wa serikali ya kaunti ya Baringo, waliosimamia shughuli ya ukaguzi wa mbuzi, waliwakataa mbuzi wake 20 hali iliyomfanya kutopata kiasi cha mapato alicholenga.

“Tuliambiwa kuwa ni mbuzi 4,000 ambao wangeuzwa katika mnada wa mwaka huu. Hata hivyo, maafisa wa kaunti walileta jumla ya mbuzi 8,700 ambao hatujui walikowatoa. Mbuzi wangu 20 walikataliwa ilhali walikuwa na afya huku waliokubaliwa walikuwa wanane pekee. Sikupata pesa za kutosha kugharamia karo ya watoto wangu,” akaeleza.

Ukora huo wa maafisa wa kaunti ulichangia bei ya mbuzi kushuka kutoka Sh18,000 hadi Sh13,000.

Zamani, machifu na manaibu wao ndio walitumika kukagua mbuzi watakaouzwa katika Mnada wa Kimalel. Mnada wa mwaka huu uliendeshwa Desemba 22, na kuongozwa na Rais William Ruto.