Akili Mali

Pacha wafurahia matunda ya mradi wao wa sungura

Na JOHN NJOROGE December 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

GIFT Waithira, 12 na pacha wake, Christine Wambui wamejitosa katika masuala ya ufugaji kutokana na mapenzi yao kwa masuala ya kilimo.

Watoto hao walionyesha ari yao wakiwa Gredi ya Tano mnamo 2023, walipoanza kuvutiwa sana na somo la kilimo.

Somo hilo ambalo ni moja ya masomo katika mtaala wa CBE, limewawezesha pacha hao kuimarisha juhudi zao.

Wakati mmoja baada ya somo hilo, Gift na dada yake walimsihi nyanya yao baada ya kutoka shuleni saa za jioni awanunulie sungura wawili.

“Nyanyangu alipendezwa na swala hilo na kutaka kujua kwa nini wazo hilo lilitoka kwetu na sababu ya msisitizo wetu juu ya swala hilo.

“Aliposikia kwamba ilikuwa kufuatia somo tulilojifunza shuleni, alifurahi sana na akaahidi kununua sungura watatu, dume mmoja na jike wawili,” akasema Gift, na kuongeza kuwa mjomba wao, Paul Maina alijenga vizimba vya sungura vilivyogharimu Sh2,000.

Kwa muda wa wiki moja, Gift alisema kwamba nyanya yao, Bi Mary Waithira alinunua sungura hao watatu kama alivyoahidi kwa Sh300 kila mmoja.

Kupitia msaada wa nyanya na mjomba waliowaahidi kuwatunza sungura hao walipokuwa shuleni, Gift ambaye sasa yuko Gredi ya Saba pamoja na pacha mwenza, walisema kwamba waliweka kibuyu chini ya jengo la sungura ili kuvuna mkojo ambao walijifunza kwamba ulikuwa mzuri na husaidia wakulima kunyunyizia kwenye mazao yao, haswa viazi, mboga za kijani kibichi, mahindi miongoni mwa mengine kwani huzuia wakulima kutokana na magonjwa na wadudu wanaovamia mazao yao baada ya kupanda.

Maneno yake yalikaririwa na Christine ambaye alihakikisha kwamba kila jioni baada ya shule, walikuwa wakiwalisha wanyama wao kabla ya kuanza kufanya kazi zao za nyumbani.

“Tuna ratiba ya kibinafsi inayotuongoza kufanya kazi zetu za shule na pia kutafuta lishe kwa sungura wetu. Tangu CBE ilipoanza,imetusaidia sisi na haswa wale ambao hawakujua umuhimu na faida ya sungura,” anasema Christine, akiongeza kuwa baada ya mwezi mmoja, sungura hao wawili walizaa wana wanane kila mmoja.

Christine alisema uzalishaji wa mkojo uliongezeka kutoka lita 15 ambazo sungura watatu walizalisha kwa wiki moja hadi lita 30 kwa wiki baada ya kuzaliwa kwa sungura hao. Alisema idadi hiyo iliendelea kuongezeka na hii ilifanya uzalishaji wao kuongezeka kila mwezi walipozaa.

Mwishoni mwa mwaka jana, pacha hao walisema sungura walikuwa wameongezeka hadi 50 na waliweza kutoa zaidi ya lita 3,000 za mkojo kila mwezi kutokana na lishe nzuri na usafi wa nyumba ya sungura ambayo mwalimu wao alisema ilikuwa muhimu sana.

“Mnamo Desemba, zaidi ya sungura 30 waliuzwa kwa kati ya Sh500 na Sh1,000 kulingana na ukubwa. Kiasi hicho kilimwezesha nyanya yangu kununua vitabu, kalamu na bidhaa zinginezo na pia kulipa karo iliyosalia tulipojiunga na Gredi ya Saba mapema mwaka huu,” anasema Gift, akiongeza kuwa mpango wao ni kupanua mradi huo ili kuvuna mkojo zaidi, ngozi na mbolea ambayo imekuwa ghali sana katika miaka ya nyuma.

Gift ambaye hucheza kandanda wakati wa mapumziko, alibainisha kuwa jengo la sungura linahitaji kusafishwa kila baada ya siku tatu na linapaswa kujengwa vizuri; kwenye nafasi iliyoinuliwa ili kuwazuia kutokana na baridi na mashambulizi kutoka kwa wanyama wengine kama mbwa.

Kwa kauli moja, wasichana hao ambao wangependa kuwa madaktari katika siku zijazo, walisema sungura hutoa mkojo zaidi wakati wa jua au joto ikilinganishwa na misimu ya baridi. Kila sungura anaweza kutoa zaidi ya lita mbili wakati wa msimu mizuri lakini hii inaweza kupungua wakati wa msimu wa baridi.

Kwa sasa, wanasema kwamba wameomba nyanya yao awafungulie akaunti ili kuwekeza pesa za ziada kwa matumizi yao ya baadaye kwani wangependa kuwa na mradi mkubwa zaidi katika siku zijazo ambao unaweza kuongezeka hadi sungura 100 ambao wangekuwa na uwezo wa kutoa zaidi ya lita 6,000 za mkojo, huku wakisema kuwa mbolea wanayokusanya inawasaidia kusimamia bustani yao ya nyumbani.

“Mahitaji ya mkojo ni makubwa sana kuliko usambazaji na hatujaweza kukidhi mahitaji ya mkulima ambayo ndio lengo letu,” anaongeza Christine, huku akipakia mkojo uliovunwa kwenye vyombo vya kuuza.

Bi Waithira, anasema mradi huo umewasaidia wasichana hao kuwa na muda mdogo wa kucheza ama kujihusisha na mambo yanayoweza kuwapotosha katika maeneo jirani.

“Kutokana na bidii yao, niliwanunulia mbuzi jike wawili ambao hutupatia maziwa kwa matumizi ya nyumbani huku ya ziada yakiuzwa kwa Sh200,” anasema Bi Waithira.